2014-07-05 16:33:24

Ujasiri, matumaini na mshikamano ni karama za vijana!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kukutana na wafanyakazi, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kupata chakula cha mchana pamoja na watu wanaohudumiwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Campobasso, Jumamosi adhuhuri, tarehe 5 Julai 2014 amekutana na kuzungumza na umati wa vijana kutoka Abruzzo na Molise kwa kuwataka kujenga matumaini pamoja na kuwa na maisha tele, yanayojikita katika njia anayoichagua kila mmoja wao kwa utulivu ili hatimaye, aweze kufikia malengo yake ya kibinadamu bila kutafuta njia za mkato.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kutafuta mambo msingi yanayodumu katika maisha yao, kwa kuwa na majibu angavu yanayoziangazia akili kwa kuonesha vipaumbele katika maisha kwani hiki ni kielelezo cha uwepo wa Mungu katika maisha yao. Vijana wanakabiliana na kishawishi cha kuogopa kukosea, kujiingiza mno katika mambo ya maisha; kishawishi cha kutaka daima kuacha uchochoro wa kukimbilia, kwa matumaini ya kuwa na mwelekeo na fursa mpya katika maisha, yote haya ni mambo yanayoutesa moyo na kuingiza giza akilini mwa vijana!

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba wanaishi katika ulimwengu ambao umegubikwa na utamaduni wa mambo mpito, ambao hautoi mwanya makini kwa ajili ya majiundo ya maamuzi fungamanishi ya maisha yanayojikita katika mwamba wa upendo na uwajibikaji na badala yake wanajikuta wakiwa wamejilaza kwenye mchanga wa hisia, majadiliano yasiyokuwa na mashiko, maamuzi mpito yanayoweza kutoweka kama ndoto ya mchana badala ya kuwa huru na kuwajibika barabara.

Mambo haya yanachangia kwa vijana kutokuwa na ukomavu wa kutosha na hivyo kujikuta wanabaki wakiwa wanaelea juu juu tu bila kuzama katika undani wa maisha, kwa kuwajibika na kuwa huru zaidi. Vijana wanapaswa kuwa na ndoto ya mambo makubwa na tunu msingi za maisha; kwa kujenga na kuimarisha urafiki unaodumu na mahusiano thabiti kati ya watu. Binadamu kwa asili ni kiumbe anayependa na kupendwa daima. Utamaduni wa mambo mpito hautaki kuunga mkono uhuru wa mtu na matokeo yake unawapokonya hatima na malengo msingi ya maisha.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuhakikisha kwamba, hakuna mtu ambaye anaweza kuwapokonya ile hamu ya kutaka kujenga maisha yao kwa kujikita katika mambo makubwa na yenye msingi. Kamwe vijana wasiridhike na mambo madogo madogo. Wanatamani kupata furaha, wawe na ujasiri wa kujitoa katika ubinafsi wao kwa kucheza vyema zaidi karata za maisha yao wakiwa wameambatana na Yesu.

Baba Mtakatifu anawahakikishia vijana kwamba, wao peke yao hawezi kufanikiwa kupata njia na mwelekeo sahihi na hata pale wanapofanikiwa wanakosa nguvu ya kudumu katika maamuzi yao ili kukabiliana na vizingiti vya maisha ambavyo hawakutegemea. Hapa Yesu anawaalika vijana kumfuasa, ili aweze kuwasindikiza katika hija ya maisha, ili pamoja na Yesu waweze kuwa na mwono mpana na nguvu ya kusonga mbele.

Vijana wengi wanasoma kwa juhudi na maarifa, lakini hawana fursa za ajira, changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na Jamii nzima pasi na kukatishwa tamaa, ili kuwasaidia vijana kukuza na kuthamini utu na heshima yao, kwa kuwajengea matumaini yanayojikita kwa kufanya kazi halali. Vijana wasiokuwa na kazi ni janga la kitaifa na kimataifa. Vijana wana matumaini, ujasiri na wana uwezo wa kujenga na kudumisha mshikamano wa dhati.

Kwa vijana Yesu atakuwa ni mlinzi, Kaka yao mkubwa na mwamuzi wa maisha yao ili kupambana na changamoto za maisha wakiwa wameungana na Yesu na Ujumbe wake, jambo linalopendeza anasema Baba Mtakatifu. Si lengo la Yesu kuwapokonya uhuru wao na kinyume chake anawaimarisha na kuwapatia uhuru wa kweli; watu huru wanaothubutu na wadumifu katika kutenda mema; vijana wenye uwezo wa kusamehe na kuthubutu kuonja msamaha.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Mwenyezi Mungu hachoki kamwe kusamehe na kufuta dhambi zao ikiwa kama watamkimbilia kwa moyo wa toba, unyenyekevu na matumaini. Anawasaidia kutokata tamaa wanapokumbana na vizingiti vya maisha, mwaliko wa kuendelea kuwa kweli na imani na matumaini, tayari kutupa tena nyavu, ili kupata samaki watakaowashangaza; vijana waendelee kuwa na ujasiri na matumaini hata katika kipindi hiki wanapokabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Ujasiri na matumaini ni karama kwa wote, lakini ni msingi wa maisha ya vijana. Maisha ya mbeleni yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kwa Yesu Kristo mwanaye wa Pekee anayewahakikishia usalama wa maisha yao. Lakini hii haina maana kwamba, vijana wafumbie macho matatizo na changamoto zilizoko mbele yao, bali wazione kama mambo ya mpito. Matatizo na kinzani kwa msaada wa Mungu na utashi wa wote yanaweza kupatiwa ufumbuzi, kushinda na kubadilishwa.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha vijana kutoka Abruzzo na Molise kwamba, katika Madhabahu ya Bikira Maria Mama wa mateso, kunako mwaka 1888 wasichana wawili yaani: Fabiana na Serafina walitokewa na Bikira Maria Mama wa Mungu walipokuwa wanalima shambani.

Bikira Maria ni msaada wa daima wakati wakati wa kazi, wanapotafuta ajira, wanapokuwa na mawazo angavu, wanapochanganyikiwa, sala zinapobubujika kama mfereji wa maji au pale wanapokaukiwa kama wakati wa kiangazi. Bikira Maria ni Mama wa Mungu, Mama wa Kanisa na Mama wa wote, mwaliko wa kumwendea na kumshukuru, kwani anawapeleka kwa Yesu na kuwakirimia amani.

Wakati huo huo, Askofu Pietro Santoro wa Jimbo la Avezzano na Mwenyekiti wa utume wa vijana, amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, vijana waliokuwa mbele yake wana matumaini na mahangaiko yao ya ndani, wanataka kukutana na Yesu, ili awasaidie katika kufanya maamuzi magumu katika maisha. Ni dhamana waliojiwekea mbele yao wakati wa sala na shuhuda kutoka kwa vijana mbali mbali kabla ya kuwasili kwa Baba Mtakatifu madhabahuni hapo. Vijana wanataka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, tayari kuwatangazia watu wa mataifa Injili ya Furaha.

Vijana kwa upande wao, wamemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wako mbele yake ili kusikiliza ushauri kutoka kwa Mchungaji wao mwema ambaye wamejaliwa na Kristo katika kipindi hiki chenye changamoto na magumu mengi, kiasi cha kuwafanya kuwa na wasi wasi kwa kesho iliyo bora zaidi. Wanakabiliana na ukosefu wa fursa za ajira na kwamba wako dhaifu kujenga mahusiano endelevu na dumifu.

Sara Messere kijana mwenye umri wa miaka 29, kwa niaba ya vijana wenzake analishukuru Kanisa kwa kuwapatia mradi unaowajengea vijana wa kusaidiana wao kwa wao ili kukabiliana na changamoto za maisha, ili kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu.

Vijana wanaupenda mkoa wao na wanataka kuona utakatifu wa maisha, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na fursa za kazi zikistawi na kushamiri kama mitende ya Lebanoni. Kwa ushuhuda wa uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko wanataka kuonesha ushuhuda wao kwa walimwengu kwamba, hata nao wamo ingawa havumi!







All the contents on this site are copyrighted ©.