Makala Dunia Mama, yanaendelea kwa mfululizo, kutafakari maisha mchanganyiko katika
jamiiya leo, kwenye ulimwengu wa utandawazi. Leo na tutazame kwa makini maisha ya
mtu mkimbizi. Je mkimbizi ni nani hasa? Na kwa nini awepo ? Je kuna manufaa yoyote
ya kuwa mkimbizi? Na jamii ifanye nini kuepusha janga la ukimbizi ?
Maana ya
"Mkimbizi" inaweza kutofautiana, lakini wengi wanakubaliana kwamba, mkimbizi ni
mtu anaye toka katika nchi yake kwa kushurutishwa na hali fulani inayotishia maisha
yake, mara nyingi ikitokana na vita, mateso ya kidini au mateso ya kisiasa. Ufafanuzi
Umoja wa Mataifa kwa wakimbizi ni "mtu yeyote ambaye: kutokana na hofu ya kuteswa
kwa sababu ya rangi, dini, utaifa, uanachama wa kikundi fulani cha kijamii, au maoni
ya kisiasa, huondoka nchini mwake na kwenda nje ya nchi yake mara nyingi bila idhini
au kwa kutoroka kwa kuwa hawawezi au, kutokana na hofu kuomba ulinzi wa nchi hiyo.
Hivyo kuna makundi au aina nyingi za wakimbizi , wakimbizi wa njaa, vita, jamii ,kidini
,kisiasa ,ubaguzi wa rangi, Kundi la kijamii, Wale walio katika hofu ya mateso hasa
wanawake na watoto.
Sheria za kimataifa za wakimbizi zinamtaja mkimbizi
kama mtu ambaye anatafuta hifadhi salama katika nchi za kigeni kwa sababu ya vita
na vurugu, au nje ya hofu ya mateso, katika nchi yake. . Pia kuna wale wanaokimbia
maeneo yao na kwenda katika eneo jingine mahali palipo salama zaidi kwa maisha yao,
nao pia Umoja wa Mataifa unawatambua kuwa ni wakimbizi.
Kwa kifupi, kuna wakimbizi
wa njaa, ambao wanatoka katika maeneo yao na kuhamia katika maeneo mengine kutokana
na ukosefu mkali wa chakula hivyo wanahama kwa ajili ya kusalimisha maisha yao ili
wasife njaa. Na wakimbizi wa dini ,ni wale wanaokimbia madhulumu ya kunyimwa haki
ya kufuata imani yao kama inavyotakiwa, mara nyingi wakinywa haki hii kwa vitisho
hata vya kuuawa, na mara nyingi watu huwa ni kundi dogo kati ya kundi kubwa la imani
moja , kama inavyo sikika sasa katika mataifa kama Pakistan, Libya, Sudan Somalia,
Wakristo wanaishi kwa hofu kubwa na wengi wao wanakimbilia sehemu zingine zenye usalama
zaidi. Aidha kuna wakimbizi wa kiuchumi, hawa hukimbia hali ngumu ya maisha nakwenda
katika nchi nyingine wanakofikiri wanaweza kuboresha hali ya maisha yao. Mara nyingi
wakimbizi hawa wa uchumi huondoka nchini mwake kwa kujiandaa taratibu si sawa na mkimbizi
wa vita, au mkimbizi wa mateso, ambaye huutumia mwanya wowote unaopatikana kuondoka
bila maandalizi. Lakini makundi yote haya huwa na tabia moja inayofanana, kuondoka
mahali wanapotakiwa kuwa na kuhamia maeneo mengine bila idhini rasmi. Ni watu wanaotoroka
toka makwao na kuingia katika maeneo mapya , kutokana na moja ya sababu zilizotajwa
hapo juu.
Leo hii tunapata habari nyingi mbalimbali juu ya wakimbizi . Habari
za wakimbizi wanao kufa maji wakijaribu kuvuka bahari kinyume cha sheria, wakimbizi
wanaokufa kwa njaa jangwani wakikimbia njaa, umaskini au maonevu katika nchi zao,
wakimbizi wanaokimbia madhulumu ya nyumbani hasa wanawake na watoto, wakimbizi wa
vita n. . Ni habari za kusikitisha na kutisha , zenye kuipenya mioyo ya watu wenye
mapenzi mema, kama Papa Francisko alivyoeleza wakati alipokitembekea kituo cha wakimbizi
cha Lampedusa Italia, Julay 8, 2013. Kituo cha Lampedusa ambacho kimekuwa mlango
maarufu wenye kupokea maelfu ya wakimbizi, wanaojaribu kuingia bara la Ulaya tokea
Afrika na mataifa mengine ya Ulaya na Asia Mashariki.
Kwa mujibu wa takwimu
za UNHCR, leo hii duniani kuna jumla ya watu zaidi ya milioni 43 wanaoishi kama wakimbizi
mahali fulani, wale waliobaki ndani ya nchi zao na wale walio hamia nchi nyingine
bila kibali. Na kwa mujibu wa shirika la Mpango wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP)
, shirika lenye kutoa hutoa msaada wa chakula kwa wakimbizi, Afrika ina wakimbizi
milioni 2.4. Wanaishi katika makambi ya 200 yaliyo tawanyika katika nchi 22, wengi
wa wakimbizi hawa ni waathirika wa vita na mateso. Shirika kwa ajili ya Wakimbizi
la Umoja wa Mataifa UNHCR kwa kushirikiana na mashirika mengine yanayo wajibika na
utoaji wa misaada ya kibinadamu kama WFP, Caritas, UNICEF, kwa makundi ya watu walio
katika mahangaiko na mateso e, huufanya kila jitihada za kuwasiliana na jumuiya ya
kimataifa kupata fedha za kulisha wakimbizi hao. Bahati mbaya mara kwa mara hukabiliwa
na uhaba wa fedha kukidhi mahitaji msingi ya kibinadamu kwa wakimbizi, wakati mwingine
hulazimika hata kupunguza mgawo wa chakula, kama ilivyo sasa, UNHCR, imelazimika
kupunguza mgao wa chakula kwa watu 450,000 wanaoishi makambini katika Jamhuri ya
Afrika ya Kati, Chad na Sudan ya Kusini kutokana na uhaba wa chakula. Na pia zaidi
ya wakimbizi 338,000 eneo la Liberia, Burkina Faso, Msumbiji, Ghana, Mauritania na
Uganda, pia wanapokea chini ya nusu asilimia 50 ya misaada wa chakula.
Mkurugenzi
wa Mpango wa Chakula (WFP), katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Bwana Ohlsen,
katika mahojiano na Redio Vatican hivi karibuni alieleza kuwa , kila mkimbizi hutumia
dola 1.5, katika gharama za msaada wa msaada wa chakula na mahitaji yake mengine
ya kila siku. Hivyo kutokana na hali hiyo, kila mkimbizi hupata mlo mmoja tu kwa
siku, ambao si wa kushibisha inavyotakiwa. . Hivyo hii ina maana watu hawa hasa vijana
na watoto wanaotazamiwa kuwa watu wazima wa baadaye ambao miili yao inahitaji lishe
bora kuijenga miili sasa miili hiyo inanyong’onyezwa na ukosefu wa lishe bora. Katika
hatua hii, wengi wana dalili wazi kama vile matumbo kuvimba, udhaifu wa mwili unaojitokeza
kama uvivu, kutopenda kazi, kuwa watu wa hasira, kuchanganyikiwa, mfadhaiko na
kushikwa na maradhi kwa urahisi. Kwenye hali hii ngumu ya kimaisha baadhi ya
wakimbizi huamua kuondoka kambini kisirisiri na kujichanganya na jamii iliyo karibu
nao, wengine hawa wanawake hujiingiza katika ukahaba, au kutumikishwa kama mtumwa
na hasa watoto, au kusajiliwa kama askari, hasa watoto na katika matukio mengine
ya kutisha, ili mradi tu aweze kupata chochote za kijikimu kimaisha.
Kwa upande
mwingine, kuna wakimbizi wanao endelea kutunza hadhi yao , na hivyo huwa tayari kushirikiana
na utawala mahalia walimo kimbilia, wakiwa tayari kuzalisha chakula chao, wakati
wanasubiri utulivu urejee katika sehemu zao . Mkimbizi mmoja katika kituo cha Lampendusa
, alimshuhudia Papa Francisco matatizo yao kwamba, wamekimbia kutoka nchi zao kwa
sababu mbili kwanza ni saba bu za kisiasa na pili ni hali mbaya ya uchumi. Na hivyo
walikuwa na hamu kubwa ya kupata mahali penye utulivu, ili waweze pia kushiriki katika
harakati za kijamii na kujiinua kiuchumi. Lakini katika harakati hizi pia kuna vikwazo
na matatizo mengi kuliko walivyotazamia. Na wala hawawezi kurudi katika nchi zao kwa
kuwa wataonekana kuwa wasaliti na hivyo heri kupambana mateso yaliyo mbele yao.
Baba Mtakatifu Francisco kwa huruma na upendo aliwatazama watu hao na kuwaambia
jinsi moyo wake unavyogusa na habari za watu wanaokufa wakiwa katika harakati za
kutaka kuokoa maisha yao. Katika hotuba yake aliwathibitishia wote bila kujali imani
yao kwamba Kanisa liko karibu na kila mmoja wa mtu anayetafuta kulinda na kutetea
hadhi ya maisha yake na familia pia .
Baba Mtakatifu alieleza na kutahadharisha
kwamba, kila mmoja wetu anaweza kuwa mkimbizi wakati wowote , pale panapotokea maisha
kutaka kudhulumika , kama ilivyokuwa kwa familia takatifu , ilikimbilia Misri kusalimisha
maisha ya mtoto Yesu aliye taka kuangamizwa na Mfalme Herode.
Baba Mtakatifu
Francisco , alimtaka kila mmoja wetu kujihoji , kuna furaha gani hasa kusababisha
mateso na dhuluma kwa ndugu yako au jirani yako, au mtu mwingine baki. Kwa nini kutaka
kutoa roho ya mwenzako ambayo huwezi kuiumba? Je wanufaika na nini unapomwanga damu
ya umwagaji wa damu yako. Papa aliendelea kusema, Mungu anauliza wote wanaofanya
madhulumu haya, Je i wapi damu ya ndugu yako anayekulilia. Ni aibu kwamba leo hii
duniani hakuna anayejisikia kuwajibika , wote tumepoteza hisia za uwajibikaji kwa
mtu mwingine, wawe wanawake au wanaume. Wote tumeanguka katika kundi la unafiki wa
Mafarisayo , kama Yesu alivyoeleza katika mfano wa Msamaria mwema . Tunawaona ndugu
zetu wake kwa waume wakiwa wametupwa pembezoni mwa barabara , na pengine twawapita
tukisema, maskini huyu, na tunaendelea na safari zetu bila kujali. Papa alionya pole
hiyo ya maneno unayoitoa bila kumwinamia mtu huyo na kusaidia inakuwa ni unafiki mkubwa.
Ni ukwepaji wa wajibu na utamaduni wa kuwajali wengine.
Papa Francisco, tangu
mwanzo wa utawala wake, hotuba zake zimeonyesha kujali sana watu masikini na wateswa.
Daima anatoa wito kwa kila Mkristu na watu wote Mwenye mapenzi mema kuwa na kujikita
katika utamaduni wa kujali na kuwafariji wengine , utamaduni wa kujiweka katika kiatu
cha mteswa na kuona jinsi makali ya uchungu wa mateso anamopita mtu huyo .
Katika
waraka wake wa Kitume juu ya Injili ya Furaha , kipengere cha tatu, anasema Kanisa
ni wazi, lenye kukaribisha kila mtu na limejaa huruma. Kanisa ni sehemu ya huruma,
wala si hukumu, kwa sababu Mungu kamwe hachoki kusamehe. Na milango yake i wazi
kwa watu wote, si kwa mahitaji si kiroho tu lakini pia hupenda kugawana lilicho nacho
kwa wahitaji wengine...
Ingawa ni kweli kwamba, pia kuna ndugu zetu wengi
wanaoishi bila urafiki na Yesu. Wengi wanaouona Ukristo kama adui. Pamoja na hatari
hizo zote Kanisa litaendelea kutangaza habari njema ya upendo na sifa chanya ya ukarimu,
heshima, huruma na uvumilivu katika uchovu wa safari inayoelekea kwenye ukomavu wa
upendo. Ni kutangaza habari inayo fungua minyororo yote ya chuki, fitina, wivu, na
dhamiri mbaya kwa watu wengine.
Hasa, Papa Francisco amebainisha kuwa, katika
umri hii ya upendo, inakuwa kigezo muhimu katika kujenga uhusiano wetu na Waislamu.
Amezitaka nchi za mapokeo ya Kiislamu ili kuhakikisha uhuru wa dini kwa Wakristo,
kama Waislamu wanavyo furahia uhuru katika nchi za Magharibi. Na ameasa dhidi ya
jaribio la kubinafsisha dini, akisema, ni kuhatarisha hali ya usalama na utulivu kwa
makundi madogo madogo yanayoonekana kuwa pinzani kiimani, Na makundi yasiyo amini
hayapaswi kuweka mikakati ya kunyamazisha imani ya waumini, iwe ni wengi au wachache.
Mafundisho haya ya Papa yanalenga kufuta sababu zote zinazoweza kumfanya mtu
kukimbia sehemu yake au nchi na kwenda kutafuta na hali palipo salama. Mama Kanisa
anaamini, kuishi pamoja kama ndugu licha ya tofauti za imani na itikadi za kisiasa,
unakuwa ni uwanja mzuri wa mmoja kujifunza mengi kutoka kwa mwingine , ni kujitajirisha
katika maelewano na urafiki miongoni mwa jamii. Ni kila mmoja kuwa mnyenyekevu wa
kumsikiliza mwingine na kujibu kwa heshima. Njia ya majadiliano ni ufunguo wa maisha
bora. Lugha chafu, vitisho na utumiaji wa silaha si jawabu katika ufanikishaji wa
maisha bora, bali hujenga utengano wenye kuyadhalilisha maisha. Matokeo yake ni uwepo
wa watu wanaozikimbia nchi zao.
Baba Mtakatifu anagusa moyo ya matatizo ambayo
hugusa maisha ya wanaume na wanawake wa leo na ambayo yana hitaji zaidi uwepo wa
Kanisa halisi. Ni lazima Injili imfikie kila mtu, bila ubaguzi kwa lengo la kujenga
amani na utulivu duniani. Papa Francisco, alionya dhidi ya watu kubaki bila msimamo
thabiti. Tunapaswa , kujenga urafiki na majirani iwe matajiri, au masikini, wagonjwa,
wale ambao ni mara nyingi hupuuzwa na kusahauliwa na jamii, watu wanaohangaika kuyaokoa
maisha yao, kama ilivyo kwa watu wakimbizi. Ni kuwa pamoja nao katika mashaka yao
yote na kuwaimarisha kwa matumaini yaliyosimikwa katika upendo wa Injili(Evangelii
Gaudium). Makala huandaliwa nami TJ Mhella.