Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 14 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa
Wapendwa wana wa Mungu, tunatafakari Neno la Mungu Dominika ya 14 ya Mwaka A wa Kanisa
Ujumbe wa leo: Mungu anajifunua kwa walio maskini, yaani waliotayari kupokea neema
na baraka zake. Tukumbuke maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya Luka yasemayo
“Roho wa Bwana yu juu yangu kwani ameniweka wakfu niwaletee maskini habari njema”
Lk 4:18.
Ujumbe huu
unajionesha wazi katika mahubiri ya nabii Zakaria kwa taifa la Waisraeli. Wako katika
utawala wa kikoloni, wamekata tamaa kwa sababu ya mateso, mashaka na manyanyaso, hawaoni
njia ya kutoka katika taabu hiyo. Nabii Zakaria mjumbe wa Mungu anatumwa kuwapelekea
habari njema ya furaha, akisema furahi sana Ee binti Sayuni, piga kelele Ee binti
Yerusalemu, tazama mfalme wako anakuja…na hivi mwisho wa taabu umefika. Anawatangazia
ujio wa Masiha mfalme wa amani atakayewaondoa katika taabu yao.
Katika tangazo
hilo la amani anawatahadharisha kuwa mfalme ajaye si wa mabavu wala wa majeshi ya
nguvu bali atakuja akiwa amepanda mwanapunda alama ya amani na ya upole. Ni mfalme
mnyenyekevu, mtulivu atakayeishi chini ya sheria ili aishinde sheria kwa ndani. Uaguzi
huu unakamilika katika Yesu Kristu Mwana wa Mungu anayekubali kuteswa na kuonewa lakini
akielekea Yerusalemu mpya.
Mwinjili Matayo anatuonesha mfalme huyu wa amani
aliyeaguliwa na nabii Zakaria akisali na kumshukuru Mungu Baba kwa kutimiza mpango
wake wa ukombozi kwa ajili ya maskini. Anasali sala ya shukrani ikiwa ni alama mojawapo
ya unyenyekevu, kifungo cha mapendo kati ya Mungu Baba na Mwana. Anafanya mawasiliano
na Baba yake akituonesha nasi kutolea shukrani kwa Mungu daima kwa njia ya sala na
majitoleo mengine mbalimbali katika maisha yetu hapa duniani.
Baada ya kutolea
sala ya shukrani anapiga tena hatua nyingine akitufundisha namna ya kumjua Mungu wa
kweli. Anasema ili kumjua Mungu Baba njia pekee ni kumjua Mwana aliye mkombozi wa
kweli. Kanisa linasadiki kina na linafundisha pasipo mashaka juu ya fundisho hili
la Kristu. Wapendwa waamini taifa la Mungu, ujuzi kamili juu ya Mungu uko katikaYesu
Kristu aliyeshuka na kupaa Mbinguni. Kristu anafundisha hili akikataa mawazo ya waandishi
na walimu wa sheria waliowakandamiza watu na kufikiri kwamba wao ndio pekee wanaoweza
kufundisha ujuzi wa kimungu kwa maskini.
Wapendwa, habari njema ya Yesu Kristu,
hatuwezi kuiishi na kuishika kina bila msaada wa Roho Mtakatifu. Mtakatifu Paulo akitambua
udhaifu wa miili ya kibinadamu anafundisha wazi kuwa miili yetu iliyo na tabia ya
kufa inahitaji kuhuishwa na Roho Mtakatifu ili iwe miili ya ufufuko. Kwa nguvu ya
Roho tuliyempokea kwa njia ya Sakramenti msingi tunapata nguvu ya kupokea fundisho
la Bwana juu ya kumjua Mungu Baba na kufuata sheria na maagizo yake.
Wapendwa
taifa la Mungu tumalizie tafakari yetu nikisema kuweni watu wa sala, sala iliyo kiunganishi
cha mapendo kati yetu na Mungu katika Utatu Mtakatifu. Tumsifu Yesu Kristu.
Tafakari
hii yaja kwenu toka kwa Padre Richard Tiganya C.PP.S.