Askofu mkuu Giancarlo Maria Bregantini wa Jimbo kuu la Campobasso-Bojano, Italia anasema
kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu Francisko mkoani Molise, Jumamosi tarehe
5 Julai 2014 ni “Mungu hachoki kusamehe”. Akiwa katika majimbo mawili, Kusini mwa
Italia, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na wafanyakazi, wananchi, wagonjwa, vijana,
wafungwa na maskini.
Maandalizi yote yamekamilika. Waamini na watu wote wenye
mapenzi mema wanaendelea kumsubiri Baba Mtakatifu Franciko ili kumwonesha upendo na
ukarimu wao. Majimbo haya mawili, yanamwomba Baba Mtakatifu Francisko, kwanza kabisa
kuwaimarisha katika imani ili waweze kuonja huruma ya Mungu.
Pili, awaombee
waamini na watu wenye mapenzi mema ili waweze kujenga utamaduni wa kukutana, ili kukuza
matumaini zaidi. Tatu: wanamwomba Baba Mtakatifu awaombee ili waweze kuwa kweli ni
watu wanaojikita katika fadhila ya upendo kwa Mungu na jirani, kwa kumthamini na kumjali
kila mtu, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Mambo haya makuu matatu
yamekuwepo kwenye sala ambayo waamini wa majimbo haya mawili wamekuwa wakisali tangu
Baba Mtakatifu Francisko alipoonesha nia na utashi wa kuwatembelea na kwamba, kauli
mbiu inayoongoza hija ya hii ya kichungaji kusini mwa Italia ni “Mungu hachoki kusamehe”.
Wananchi wanataka kusikiliza Baba Mtakatifu Francisko atawaambia nini wafanyakazi
wanaoendelea kuathirika kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.
Wananchi
wanakabiliwa na ukosefu wa fursa za ajira kiasi cha kuwafanya watu wengi kukosa matumaini
ya kesho iliyo bora zaidi na kwamba, utu na heshima yao kama binadamu iko mashakani.
Waamini wanamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaonesha njia ya kufuata kwa ajili ya
vijana ambao wanaonekana kukosa dira na mwelekeo wa maisha, kama ilivyo kwa vijana
wengi duniani kwa sasa!
Askofu Camillo Cibotti wa Jimbo Katoliki Isernia-Venafro
anasema, tukio kubwa linalotarajiwa kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati
wa hija yake ya kichungaji ni kutangaza Mwaka wa Jubilee wa Papa Celestini, tangu
kuzaliwa kwake kunako mwaka 1215. Mwaliko wa jumla ni kuonesha mshikamano wa upendo
na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; kwa kusimama kidete
kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu. Kimsingi mwanadamu anapaswa kupewa
kipaumbele cha kwanza katika mikakati ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Baba
Mtakatifu Francisko anatembelea Jimbo Katoliki la Isernia ambako tarehe 5 Julai 1294
Papa Celestini alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, hapa kuwa ni sherehe kubwa
kwa Jimbo zima kwani mtoto wao alikuwa amechaguliwa kuwa Papa.