Yesu alipoanza maisha yake ya hadharani baada ya miaka yapata thelathini hivi ya umri,
alihama toka nyumbani kwake Nazareti akaenda kukaa sehemu inayoitwa Kafarnaum, kando
ya ziwa la Galilea na hakurudi tena Nazareti. Hoja kuu za kuhama Nazareti zilisababishwa
na wakazi wake.
Hao walikuwa watu wa kufuata mno mila na desturi, yaani, hawakuwa
tayari kupokea mabadiliko katika maisha hata baada ya kuona ishara za nyakati zinazodai
kufanya mageuzi ya maisha. Huko Kafarnaum kwa mwanzoni mambo yalimwendea vizuri, yaani
watu walimpokea kwa hamasa kubwa, lakini ilikuwa kama wasemavyo wahenga “mbuzi mgeni
wachungaji wengi”.
Baada ya kupita kitambo kifupi hata huko nako kukaanza
kujitokeza mizengwe. Upepo wa mbisho ukamgeukia Yesu kiasi cha kupoteza wafuasi wake
wengi: “Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma” (Yoh
6:66).
Mbaya zaidi hata ndugu zake kabisa wa ukoo, akiwamo Mama yake mzazi
walisafiri toka Nazareti hadi Kafarnaum kuja kumchukua wakidhani amechanganyikiwa.
“Wakaja mamaye na nduguze; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita. Na makutano walikuwa
wameketi, wakimzunguka; wakamwambia, “Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”
(Mk 3:31-32).
Hoja ni kwamba, hata huko Kafarnao, lugha na mapendekezo aliyotoa
kwenye heri nane ilikuwa ngumu kwa watu kupokea na kufuata. Ingawaje kulikuwa na mafanikio
ya hapa na pale yaliyotokana na hotuba zake na miujiza kadhaa aliyofanya huko, lakini
mwitiko hasi wa watu ulimchanganya Yesu na akawa haelewi kwa nini hawampokei kirahisi.
Kutokana
na hali hii, wakati mwingine ilimlazimu kuikaripia miji mbalimbali alimoisha hubiri
na kufanya miujiza, na wasikilizaji wake walibaki hamnazo kama walioziba masikio.
Yaani watu hawakubadilika katika fikra na hawakuonesha kuongoka. Katika miji wanamokaa
watu aina hiyo hakuchelea kuiambia ukweli: “Ole wako Korazini, Ole wako Betsaida”
(Mt 11:21). Ole hii, haikuwa na maana ya kulaani, bali ilikuwa ni ya tahadhari ambayo
mmoja anapaswa kuwa nayo mbele ya maisha, hasahasa mbele ya kifo. Ni kama vile alitaka
kuwaambia: “Jamani tafadhali jihadhalini!”
Katika hayo yote swali nyeti alilokuwa
anajihoji Yesu ambalo hata sisi tungeweza kujiuliza ni hili: “Kwa sababu gani hali
iko hivyo.” Yaani baada ya Yesu kujitoa nguvu zake zote kufundisha, kuhubiri, kuponya
nk, matokeo yake ni kukataliwa, na watu kutokujali chochote wala kubadilika, tungeweza
kusema: “wanamshiti.” Kibinadamu mambo yanapoenda kinyume na mategemeo yako, mtu unaweza
ukakata tamaa kwani huoni mafanikio ya juhudi na nia zako njema.
Hali kama
hii yaweza kumtokea kila mmoja wetu, hususani mzazi, mwalimu au hata kwa kiongozi
yeyote yule, anayejitoa nguvu zake zote kuwasaidia wenzake, kuwafundisha, kuwalea,
kuwahangaikia kwa namna yeyote iwayo, lakini matokeo yake yanakuwa ni kukataliwa,
kuchukiwa na pengine hata kushtakiwa. Hapo mtu unabaki kujihoji bila kupata jibu,
kulikoni! na hujui ufanye nini katika hali kama hiyo. Njia wanayotumia wengi ni kuyakimbia
mazingira hayo kwa muda na kwenda likizo, au kwenda kujiburudisha kwa namna yoyote
ile, na kama hayawezekani kuyatoroka mazingira unabaki kukata tamaa na wengine huamua
hata kujinyonga.
Hebu tuone jinsi Yesu anavyoikabili hali hiyo, yaani mambo
yanapomwendea kombo. Kwanza kabisa Yesu anazisoma kwanza ishara za nyakati. Namna
anavyosoma mazingira ni tofauti na tufanyavyo sisi. Baada ya kuona mwenendo wa mambo
unavyoenda, mbinu anayochukua Yesu ni kwenda pahala pa mficho peke yake na kusali.
Lengo la kwenda pahala pa pekee na kusali ni kutaka kuangalia katika mwanga
wa kioo ambacho ni Mungu Baba yake, ili katika mwanga huo aweze kuisoma vizuri zaidi
ishara hizo za nyakati na kuelewa maana halisi ya matatizo yanayomtokea. Sala siyo
kwa ajili ya kupata neema fulani, au kwa ajili ya kumshawishi Mungu akutendee jambo
fulani kadiri unavyotaka wewe, la hasha, bali Yesu alitaka aone katika mwanga wa Mungu
ni ishara ipi ya nyakati ipo katika vituko hivyo vya kusikitisha anavyovishuhudia
vya kukataliwa ujumbe wake. Baada ya kuona uhalisia huo wa mambo anasali: “Nakushukuru
Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili,
ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako”
(Mt 11:25).
Yesu anaanza kwa kumshukuru Baba yake. Kushukuru maana yake
ni kutambua, kukiri, kusifu, kuungama kwa furaha mwanga, ufahamu na utambuzi alioweza
kuupata kwa kuonana na Baba. Kwamba sasa ametambua sababu za kukataliwa kwake au sababu
za mgomo na za watu kumshiti, licha ya harakati na kazi yote aliyofanya katika kutafuta
kuwashirikisha watu mwenendo wa maisha. Hivi ndivyo anavyoingia katika majadiliano
na Mungu ili kupata mwanga wake zaidi.
Katika injili unalikuta neno hili “Baba”
yaani jinsi ya kumwita Mungu linajitokea mara 182. Aidha neno hili linatamkwa na Yesu
tu, na kwa mara moja lilitamkwa na Filipo anapomwomba Yesu: “Bwana utuoneshe Baba
yatutosha” (Yoh 14:8). Kumbe, mara nyingi Yesu anaposali analitumia jina hili Baba,
au Abba, Dady, “Tata”! Katika fasuli ya Injili ya leo, unalisikia neno hili “Baba”
linatamkwa mara tano likionesha mahusiano ya karibu sana na ya umwandani kati yake
na Mungu. Marabi wa Kiyahudi hawakulitumia wanalitumia jina hilo, kwa sababu siyo
neno la kiutu uzima na lenye hadhi, bali ni la kitoto, yaani ni jina la kimapendo
linalotumika na mtoto katika kumwita baba yake ampendaye sana, Dady!
Kumbe
Yesu ametaka tulitumie jina hilo kumwita Mungu, kwa vile Mungu wetu siyo wa kutisha,
bali Mungu ni mapendo, anayetupenda na kutusaidia kama watoto wake wapendwa. Hivi
hapa Yesu anatujulisha mahusiano ya upendo aliyo nayo yeye na Baba yake. Anatualika
sisi tuwe na mahusiano hayo hayo na Mungu kama ya mtoto mdogo kwa baba yake mpendwa.
Yesu anatambua kwamba huyu Mungu ndiye anayeongoza ulimwengu kwa namna ya pekee. Anataka
tuelewe mantiki hii mpya ya mahusiano yetu na Mungu.
Kitu alichogundua
Yesu katika sala ni kuwa mambo hayo yote aliyoyafanya Yesu, kumbe Mungu ameyafunua
kwa watoto wadogo, “Mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto
wachanga.” Huu ndiyo ukweli aliokuja kuugundua Yesu katika sala, kwamba Mungu ameufunua
ukweli huo mkuu kwa watoto wadogo.
Kumbe ndugu zangu, wenye hekima na akili
wanajiona wamekamilika, wameridhika na maisha yao, na maraharaha waliyo nayo. Mabadiliko
na mambo hayo mapya ya Yesu Kristu yanawaletea vurugu. Wanajitosheleza, kama vile
ilivyokuwa kule Nazareti alipojaribu kurudi mara moja, hawakumpokea tena, hata akawaambia:
“Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na
nyumbani kwake” (Mark 6:4). Watu hao wenye hekima wanataka kushikilia mapokeo yao
na hawataki mabadiliko ya mambo hata baada ya kuona ishara za mabadiliko ya nyakati.
Hawa ndiyo wenye hekima hata kama hawajui kusoma na kuandika lakini wanajua yote.
Tunawapata watu namna hiyo katika maisha yetu, yaani watu wale wasiotaka kusoma,
kutafakari biblia na kuona mabadiliko yaliyoko katika biblia. Watu wasioweza kusoma
ishara za nyakati, hao ndiyo wanaojifanya mafundi wa kumkashifu Kristu. Huo ni mwaliko
kwetu wa kuwavumilia na kuwaheshimu watu wa aina hii. Aidha huo ni mwito hata kwa
viongozi wa kila aina, wakiwepo wale wa serikali, wa siasa na wa dini zozote zile,
hususani kwa wazazi wanaotoa nguvu zao zote kusoma ishara za nyakati na kuwafundisha
au kuwaonesha watoto wao uupya wa maisha. Lakini wao hawaelewi au wanaziba masikio
yao.
Hao watoto wadogo anaowatamka Yesu, haina maana ya wale wasiojua,
bali ni wale wasiojitoshelesha na wanaojua kwamba wakitaka furaha ya kweli wapokee
fikra za Bwana wa Nazareti. Ujumbe wa Yesu na ufunuo wake ni zile heri nane. Alichokitegemea
Yesu ni kuwa wataalamu na wenye hekima ndiyo wangezielewa na kuzipokea hizo heri nane
na kuzifanyia kazi. Kumbe kinyume chake wao walizibeza. Kumbe sasa Yesu anatambua
kuwa hayo ndiyo mambo yaliyokuwa katika mipango ya Mungu.
Mara nyingi tunalalamika,
tunataka mambo yaende kama tunavyotaka sisi. Yesu anatualika kuangalia mambo kwa namna
alivyofanya Yeye. Tuangalie mambo na kuishi maisha kwa utulivu na kumtegemea Mungu
hasa mambo yanapotuendea kombo. Aidha, Yesu anatualika kuwapokea watu jinsi walivyo
hata kama watu hao hawapokea mwito wa Mungu, tuone mambo vizuri, tuishi kwa utulivu.
Yesu anatambua kwamba kukosekana kwa roho hiyo kunaweza kutusababishia kukata tamaa.
Yesu
anaendelea na sala: “Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana,
ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia.”
Huo ni mwito wa kuingia kwenye umoja na shukrani hii kwa Baba, inavyooneshwa na Yesu
katika uchaguzi tunaotakiwa kuufanya. Kisha Yesu anatualika anasema: “Njoni kwangu,
ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Wanaalikwa
kupumzika kwa sababu wamekabiliwa wamebebeshwa na mizigo mizito.
Ni wale waliokuwa
wameshinikizwa na mafundisho ya wale wanaojidai kuwa ni wenye hekima na akili, waliochukua
hadhi ya kuwa mababa wa kiroho, wamechukua hadhi ya Mungu, wanajidai kuwa ni miungu
na wenye kutunga na kufuata sheria nyingi. Yesu anawaalika hao watoto wadogo kubeba
mzigo wake ambao ni mwepesi.
Kwa kawaida mzigo huo ni yale magogo yanayofungwa
kwenye shingo au mabega ya ngombe na kufungiwa mzigo. Mara nyingi hubebwa na ng’ombe
wawili. Maana yake sasa nira hiyo itabebwa na wawili, yaani Yesu Kristu pamoja na
kila mmoja wetu. Mzigo huo siyo mzito bali ni mwepesi kwa sababu unatokana na hadhi
tuliyo nayo ndani yetu, yaani inatudai tuwe wenyewe, tujipokee jinsi tulivyo kwani
tunabeba pamoja na Yesu.
Nira hiyo ni unyenyekevu ambao Yesu anatualika tuungane
naye aliye mpole na mnyenyekevu. “Njoni kwangu mimi niliye mpole na mnyenyekevu wa
moyo.” Wale walio tayari daima kujipokea na kusema: “haya ndiyo maisha”. Hali na mtazamo
wa kutoa maisha kwa ajili ya ndugu. Hali ya kupenda kutokana na hali ya ndani ya Kristu
iliyo ndani yetu. Ukipokea ndani mwako unyenyekevu wa Yesu, utaweza kujitenga pembeni
na kujitazama katika kikoo cha Mungu kwa sala, na utafanikiwa kusoma kwa unyenyekevu
ishara zote za nyakati na kuzipokea, na hatimaye hutakata tamaa bali utasali daima
kama Kristu: “Nakushukuru Baba”.