Jubilee ya miaka 500 tangu alipozaliwa Mtakatifu Theresa wa Avila
Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwa Majimbo yote Katoliki nchini Hispania kuadhimisha
Mwaka wa Jubilee ya miaka mia tano tangu alipozaliwa Mtakatifu Theresa wa Avila, maadhimisho
ambayo yataanza kutimua vumbi tarehe 15 Oktoba 2014 na kuhitimishwa rasmi hapo tarehe
15 Oktoba 2015.
Katika maadhimisho haya, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Hispania amepewa kibali cha kutoa rehema na baraka za kipapa kwa waamini wote watakaoshiriki
katika maadhimisho haya kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa ili kumwezesha
mwamini kupata rehema kamili. Kwa waamini wanaotaka kupata rehema kamili, itawabidi
kushiriki Ibada ya Misa Takatifu, kuungama, kupokea Ekaristi Takatifu na kusali kwa
ajili ya nia ya nia za Baba Mtakatifu.
Mtakatifu Theresa wa Avila anayejulikana
kama Theresa wa Yesu alizaliwa kunako tarehe 28 Machi 1515 huko Avilla, Hispania.
Akiwa na umri wa miaka ishirini, alijiunga na Shirika la Watawa wa Karmeli, baada
ya tafakari na hija ya maisha ya ndani aliyoifanya kwa kipindi cha miaka thelathini
na tisa, aliweza kufikia wongofu wa ndani, akawa ni kati watu mashuhuri kabisa ndani
ya Kanisa waliojikita katika mchakato wa mabadiliko ndani ya Kanisa, kwa maandiko
lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wake wa maisha.
Mtakatifu Theresa wa Avilla
akawa ni chachu ya maisha ya kitawa sehemu mbali mbali nchini Hispania. Akafariki
dunia tarehe 15 Oktoba 1582. Akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Paulo V kunako mwaka
1614. Papa Gregorio XV kunako mwaka 1622 akamtangaza kuwa Mtakatifu. Mtumishi wa Mungu
Papa Paulo VI kunako mwaka 1970 akamtangaza na kumwandika katika Orodha ya Walimu
wa Kanisa Katoliki pamoja na Mtakatifu Katarina wa Sienna.