2014-07-04 08:49:32

Familia zijengewe uwezo kukabiliana na changamoto za maisha!


Vitendo vya jinai na unyanyasaji vinavyofanywa dhidi ya watoto wadogo ni sehemu ya litania ya mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya watoto kwa sasa na kwa siku za usoni. RealAudioMP3

Kuna utalii wa ngono unaowahusisha watoto wadogo, picha za ngono, mauaji ya watoto wenye ulemavu wa ngozi, watoto wanaofanyishwa kazi za suluba na kupelekwa mstari wa mbele wakati wa vita na machafuko ya kisiasa. Haya ni mambo yanayohitaji kujenga utashi wa kisiasa, ili kuchukua hatua madhubuti kuanzia katika ngazi ya mtu binafsi, Jamii, Taifa na Kimataifa, ili kuweza kukabiliana, kuyashughulikia kisheria na hatimaye, kuyang’oa katika Jamii.

Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na biashara haramu ya binadamu inayoendelea kushamiri kila kukicha jambo ambalo ni kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Utumwa mamboleo ni biashara ya kitaifa na kimataifa inayowaingizia wahusika mabillioni ya fedha. Baadhi ya watu wanajikuta wametumbukizwa katika biashara hii kwa kupewa ahadi za uwongo, kwa kutamani kupata maisha bora zaidi au fursa za ajira, lakini mwishoni, wanajikuta wakiuzwa kama bidhaa sokoni.

Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya upembuzi yakinifu ili kupata kiini cha matatizo haya ili kuyapatia ufumbuzi wa kudumu. Watoto wengi wanajikuta wakinyanyaswa na kudhulumiwa utu na heshima yao kutokana na: umaskini wa hali na kipato wa familia zao; athari za myumbo wa uchumi kimataifa; kinzani za kisiasa, kikabila na kidini; mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kwa watoto kujikuta wanakosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha.

Ni mchango kutoka kwa Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva wakati wa mkutano wa Baraza la haki msingi za binadamu la Umoja wa Mataifa, uliofanyika hivi karibuni mjini Geneva. Anasema, kwa miaka kadhaa Vatican imeonesha wasi wasi wake kutokana na madhara ya kuvunjika kwa ndoa na familia nyingi duniani na kwamba, wanaoteseka zaidi ni watoto. Familia nyingi zinakabiliana na matatizo makubwa kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake.

Kutokana na changamoto hizi, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati na sera makini kwa ajili ya kujenga na kuimarisha misingi bora ya familia pamoja na kuzijengea familia uwezo wa kiuchumi ili kukabiliana na gharama ya maisha. Mikakati hii ikitekelezwa kwa umakini mkubwa inaweza kusaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya kifamilia, madhulumu na nyanyaso kwa watoto wadogo na wanawake.

Ujumbe wa Vatican unaendelea kukazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu sheria za kimataifa kuhusu watoto wadogo kupelekwa mstari wa mbele katika vita na migogoro ya kijamii. Ni jambo lisilokubalika kuona kwamba, watoto wanapelekwa mstari wa mbele kuwa ni chambo cha mapigano. Inasikitisha kuona kwamba, watoto wanapokonywa matumaini ya maisha bora kwa sasa na kwa siku za usoni, kwa kulazimishwa kwenda Jeshini, kutekwa nyara, kujeruhiwa na hatimaye kufa wakiwa vitani!

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.