2014-07-03 10:00:49

Wasaidieni Maaskofu kutekeleza wajibu wao!


Padre Tumaini Ngonyani Litereku kutoka Jimbo kuu la Songea ni kati ya wawakilishi waliofika kwenye Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume, Ibada ya Misa takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini vatican, Jumapili tarehe 29 Juni 2014 pamoja na kutoa Pallio takatifu kwa Maaskofu wakuu 27, kati yao akiwemo Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la songea, Tanzania. RealAudioMP3

Padre Litereku katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, kilichomgusa zaidi ni ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Familia ya Mungu kwa kuwahimiza wakristo wote kuwa ni mashahidi wa Kristo pasi na woga, wawe tayari kutoka kimasomaso kumtangaza na kumshuhudia Kristo mahali popote pale walipo!

Padre Litereku anasema, Pallio takatifu ni alama ya mshikamano na umoja kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu wakuu wanapotekeleza dhamana na utume wao kwenye Majimbo kuu. Ni kielelezo cha Kristo mchungaji mwema anayejisadaka kwa ajili ya Kondoo wake, ili kuwatafutia malisho mema. Ni alama pia ya Kondoo wanaobebwa na Maaskofu wakuu, changamoto kwa waamini kujitahidi kutokuwa ni mizigo mizito ambayo itawaelemea Maaskofu kiasi cha kugumisha utekelezaji wa majukumu yao.

Padre Tumaini Ngonyani anasema, kila mwamini anapaswa kutekeleza dhamana, wajibu na wito wake wa Kikristo, ili Maaskofu mahalia waendelee kutekeleza dhamana yao ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu na kwa njia hii, watakuwa tayari kuwawezesha na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao ya Kikristo hapa duniani.

Padre Tumaini anasema, Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea ana matumaini makubwa kwa waamini kutoka Jimboni humo na kwamba, anaamini kwamba, watashirikiana kwa pamoja katika ujenzi na ustawi wa Jimbo kuu la Songea, kiroho na kimwili!







All the contents on this site are copyrighted ©.