2014-07-03 11:06:47

Jiandaeni kiroho kwa ujio wa Papa Francisko!


Askofu mkuu Giancarlo Bregantini wa Jimbo kuu la Campobasso-Bojano, Italia, anawakumbusha waamini kwamba, Jimbo lao limesimikwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, changamoto kwa waamini kujifunza kusema, asante, kwani Ekaristi Takatifu maana yake ni Shukrani na changamoto ya kusimamia mema na kujenga urafiki, upendo na mshikamano wa kweli kwa kujitoa kwa ajili ya wengine ndani ya Jamii.

Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu kwa kuendeleza ari na moyo wa ushirikiano, wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko anayetarajiwa kutembelea Jimboni humo, Jumamosi ijayo, tarehe 5 Julai 2014. Kwa namna ya pekee, waamini wanaalikwa kujiandaa kiroho kwa ajili ya kumpokea Baba Mtakatifu, kwa kuonesha ukarimu na mshikamano na maskini pamoja na wahamiaji.

Askofu mkuu Bregantini anawataka kushikamana na kuonjeshana umoja wa kweli, kwani Baba Mtakatifu anapenda kuwakumbatia wote ili kuwaonjesha huruma na upendo kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa maneno machache, waamini wajiandae kikamilifu kumpokea na kumwonesha moyo wa upendo na ukarimu Baba Mtakatifu Francisko anapotembelea Jimboni humo!







All the contents on this site are copyrighted ©.