Kardinali John Onaiyekan Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria anasema, watu
wamechoshwa na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram; wananchi
na watu wenye mapenzi mema wanataka amani na utulivu, mambo msingi katika kukuza na
kudumisha maendeleo ya watu kiroho na kimwili.
Wananchi wanataka
kuona kwamba, uhuru wa kuabudu unaheshimiwa na kuthaminiwa na wote na kwamba, haki
inashika mkondo wake bila kigugumizi chochote.
Kardinali Onaiyekan anasema,
ikiwa kama kweli Boko Haram wanataka amani na upatanisho; wanataka kusitisha mashambulizi
na nyanyaso na utekaji wa watu wasiokuwa na hatia, basi kuna haja ya kuanzisha mchakato
wa majadiliano yanazozingatia ukweli na wote wanaoendelea kusababisha mashambulizi
kwa watu wasiokuwa na hatia.
Inawezekana kabisa hata katika hali kama hii
ambayo inaonesha kwamba watu wengi wamekata tamaa na wangependa kulipiza kisasi kwa
kuhakikisha kwamba, Kikundi cha Boko Haram kinaoneshwa cha mtema kuni, lakini ukweli,
upatanisho wa kitaifa na msamaha ni mambo yanayowezekana, ili Nigeria iweze kujikita
tena katika amani na upatanisho, kwani chuki na dhana ya kulipizana kisasi itaendeleza
machafuko na kinzani nchini humo pasi na suluhu ya kweli.
Serikali ya Nigeria
na vyombo vya usalama wa taifa zimewekeza rasilimali watu na fedha kwa ajili ya kupambana
na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, lakini matokeo yake ni watu bado wanaendelea
kutekwa nyara, kuuwawa kikatili na kuchomewa nyumba zao. Msamaha unaweza kutolewa
kwa wale ambao watakana na wala hawatajihusisha tena na vitendo vya kigaidi, ili kuanza
maisha mapya.
Boko Haram wanapokamatwa, wanashitakiwa na kuhukumiwa kifo,
matokeo yake ni kuongeza chuki na uhasama kati ya watu wasiokuwa na hatia. Hali kama
hii ikiendelea hivi, hakuna uwezekano wa Kikundi cha Boko Haram kujisalimisha na hivyo
kuanza mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Chuki,
vita na uhasama ni cheche ambazo zitaendelea kuwavuruga wananchi wa Nigeria.
Kwa
watu wanaotaka kuanza mchakato wa majadiliano ni alama wazi kuwa wanataka kuleta walau
ufumbuzi wa tatizo ambalo linaendelea kusumbua vichwa vya watu wengi ndani na nje
ya Nigeria. Kwa wale wanaotaka kugeuza maisha yao kwa kuachana na vitendo vya kigaidi,
watendewe kwa haki na kwamba, watu walioathirika kwa vitendo vya kigaidi walipwe fidia!
Wazo kama hili la kufanya majadiliano na Kikundi cha Boko Haram liliwahi kujitokeza
na Serikali ya Nigeria ikaonekana kana kwamba, imekunwa kidogo na wazo hili na kutaka
kuridhia, lakini baada ya kushutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa kwamba, Nigeria inajadiliana
na Magaidi, ikabadili msimamo wake na kusema kwamba, Serikali ya Nigeria itakula sahani
moja na magaidi, hadi pale kitakapoeleweka! Hapa ni falsafa ya jino kwa jicho inayotawala!