Changamkieni teknolojia ya habari katika Uinjilishaji!
Askofu Bernadin Mfumbusa, Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano, Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania anawahimiza wanahabari wakatoliki kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kutumia
kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia katika sekta ya habari ili kuwatangazia
watu Injili ya Furaha kwa uhakika Zaidi.
Askofu Mfumbusa ameyasema hayo, Jumatatu
tarehe 30 Juni 2014 wakati alipokuwa anafungua warsha ya siku tatu ya mawasiliano
kwa wajumbe kutoka katika Nchi za Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
Mashariki na Kati AMECEA, kwenye Kitivo cha Mawasiliano ya Jamii, Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Augostino cha Tanzania, SAUT, huko Msimbazi, Jijini Dar es Salaam.
Askofu Mfumbusa
amewataka wanahabari Wakatoliki kwenda na wakati kwa kuchangamkia matumizi ya njia
za mawasiliano ya kisasa, ili kuchangia kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji
mpya, unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Kanisa kwa miaka mingi Barani
Afrika limekuwa nyuma katika matumizi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano
ya jamii.
Umefika wakati kwa wanahabari wa Kikatoliki kutumia mitandao ya
kijamii ili kuweza kupanua wigo wa mawasiliano na watu mbali mbali duniani. Askofu
Mfumbusa anasema, leo hii kuna simu za kiganjani zipatazo billioni 5. 9 zinazotumika
kila siku kukicha, njia hizi pia zinaweza kutumiwa na Kanisa Barani Afrika ili kuwatangazia
watu Habari Njema ya Wokovu. Kuna watu wengi Barani Afrika wanaoendelea kutumia mitandao
ya kijamii, mapinduzi makubwa yanayojionesha Barani Afrika.
Warsha hii iliwahusu
zaidi waandishi wa habari wanaotekeleza dhamana yao kwenye mitandao na imeandaliwa
na Idara ya Mawasiliano ya Jamii, AMECEA na inawashirikisha wajumbe kutoka Sudan ya
Kusini, Malawi, Zambia, Kenya, Uganda na Tanzania.