2014-07-02 11:09:34

Watanzania wanahitaji Katiba Mpya!


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Julai Mosi, 2014 ameadhimisha kilele cha Jubilee ya miaka 25 ya uaskofu na miaka 40 ya Upadre, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na Familia ya Mungu nchini Tanzania. Waziri mkuu Mizengo Pinda alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sherehe hizi zilizofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa Kanisa kuu la Kihesa, Jimbo Katoliki Iringa.

Mahubiri yametolewa na Askofu mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora. Askofu Severin Niwemuzi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, katika salam za Baraza la Maaskofu, amewataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kurejea kwenye mkutano wake uliopangwa kuanza tarehe 5 Agosti 2014, ili kuwapatia watanzania Katiba inayofaa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uzalendo na ikiwa kama Katiba Mpya "itachakachuliwa" basi watanzania waikatae wakati wa kupiga kura ya maoni pamoja na kuwanyima kura viongozi wote watakaokwamisha mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Tanzania.

Askofu Niwemugizi amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la wapiga kura wakati utakapowadia na kuachana kabisa na tabia ya kudharau mambo ya kisiasa kwani yanagusa maisha yao na ya watanzania wengine wote. Anasema, huu ni wakati wa kuliombea Taifa la Tanzania ambalo kwa sasa limegawanyika, kwa baadhi ya watanzania kuhodhi rasilimali na utajiri wa taifa wakati watanzania wengine wakiwa wanaogelea katika lindi la umaskini. Mchakato wa kuandika Katiba umewagharimu sana watanzania na sasa wanataka kuona matokeo yake kwani Katiba mpya ndiyo itakayotoa mwelekeo wa Tanzania na wananchi wake.

Akizungumza katika Sherehe hizi, Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amewaomba viongozi wa dini nchini Tanzania kuombea amani na utulivu wakati wa uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani, ili Taifa liweze kuwapata viongozi ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote; viongozi ambao wanajipambanua kwa kuwa na maadili na utu wema. Waziri mkuu anasema kwa sasa rushwa, ubinafsi na tabia ya baadhi ya viongozi kutowajali wananchi ni janga la kitaifa.

Amewataka watanzania kudumisha moyo wa kupendana, kuheshimiana na kuvumiliana, ili kufanikisha mchakato wa kupata Katiba Mpya na hatimaye, wananchi waweze kuipigia kura ya maoni kama fursa ya kutoa maamuzi ya mwisho. Sherehe hizi zimehudhuriwa pia na Rais mstaafu Benjamini Mkapa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Anne Makinda pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Kisiasa kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Iringa.







All the contents on this site are copyrighted ©.