Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la wahamiaji na watu wasiokuwa
na makazi maalum anasema kwamba, kuna watu wanaendelea kufa maji katika Bahari ya
Mediterrania, wakiwa na tumaini la kupata maisha bora ugenini.
Bara la Ulaya
ni tumaini la wahamiaji wengi wanaoendelea kuhatarisha maisha yao kwa kukabiliana
na hali ngumu jangwani na baharini, wachache wanafaulu kutua nanga ya matumaini, lakini
kuna maelfu ya watu ambao wamepoteza maisha yao Jangwani na Baharini, wakiwa kwenye
harakati za kuelekea Ulaya. Ni watu wanaozikwa kwenye makaburi yasiyokuwa na Misalaba
chini ya Bahari.
Mitumbwi na mashua wanazotumia badala ya kuwapatia matumaini
mapya ya maisha anasema Kardinali Vegliò imekuwa ni majeneza ya kuwasindikiza kwenye
kina cha bahari. Hivi ndivyo alivyosema Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea kwa
mara ya kwanza Lampedusa hapo tarehe 7 Julai 2013, ili kushuhudia kwa macho yake mwenyewe
mateso na mahangaiko ya wahamiaji, ambao wanaendelea kuweka rehani maisha yao wakiwa
na matumaini ya kupata maisha bora zaidi.
Hawa ni watu wanaokimbia vita, nyanyaso
na madhulumu; ni watu ambao wameonja adha ya maisha kutokana na umaskini wa hali na
kipato; ni kundi la watu waliokata tamaa kutokana na kinzani za kidini, kijamii na
kisiasa, kiasi kwamba, kwao maisha hayana thamani tena, hata kama watazama maji na
kupotelea tumboni mwa bahari kwao si jambo la kuhuzunisha tena!
Hata pale wachache
wanapofanikiwa kutua nanga ya matumaini kwa kufika Barani Ulaya, wanakumbana na sheria
kali na baguzi, zinazowatenga na kuwanyanyasa kana kwamba, hakuna sheria za Kimataifa
zinazosimamia na kuratibu hali ya wakimbizi na wahamiaji duniani.
Watu wa
Ulaya inaonekana wamechoka kusikia kila wakati maafa ya wahamiaji na wakimbizi wanaopoteza
maisha yao huko Jangwani na Baharini, wanasahau kwamba, watu ambao wameokolewa maisha
yao ni tumaini kwa familia na jamii inayohusika.
Kardinali Vegliò anasema
kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu makini zinazolinda na kudumisha
utu na heshima ya binadamu. Kwa wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya kisiasa wasipewe
mgongo, wasaidiwe kulingana na sheria na kanuni za kitaifa na kimataifa.
Kardinali
Vegliò anawataka wakimbizi na wahamiaji wasithubutu kuhatarisha maisha yao kwa kujikabidhi
mikononi mwa watu ambao wanauchu wa mali na utajiri wa haraka wanaowaahidia fanaka
na maisha yenye raha ughaibuni, lakini wanasahau kwamba, wanawadanganya na kuwalaghai
na wala ukweli haumo ndani mwao. Hii ni safari inayofanywa hata na watoto wadogo na
wanawake wanaotembea na kifo miguuni pao!
Ni watu wasiokuwa na matumaini kwani
mara nyingi watu kama hawa wanatumbukia katika mikono ya wafanyabiashara haramu ya
binadamu au watu wanaojihusisha na utumwa mamboleo, kiasi kwamba, watu hawa wanaendelea
kuteseka kiroho na kimwili na kwamba, utu na heshima yao havina thamani tena.
Kardinali
Antonio Maria Vegliò, katika Ibada kwa ajili ya kuwaombea wahamiaji na wageni wanaokufa
maji wakiwa njiani kwenda Barani Ulaya iliyofanyika hivi karibuni kwenye Kanisa kuu
la Bikira Maria wa Trastevere mjini Roma, anasema kwamba, kuna haja kweli ya kujenga
na kudumisha utamaduni wa ukarimu kwa nchi za Ulaya, ili kweli Bahari ya Mediterrania
iwe ni kielelezo cha matumaini, amani, upendo na mshikamano! Mahali ambapo watu wanaweza
kusikia tena wakisalimiana, amani kwako, shallom, salam alay kum, pax vobiscum!
Imehaririwa
na Padre Richard a. Mjigwa, C.Pp.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.