2014-07-01 08:56:24

Wao! Wazee kukutana na kuteta na Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 28 Septemba 2014 anatarajiwa kukutana na kuzungumza na wazee, mababu na mabibi kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha marefu yanayoliwezesha kundi hili kuweza kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu.

Tukio hili linatarajiwa kuanza majira ya saa 1:30 asubuhi kwa wazee kuanza kuingia kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na Ibada ya Misa Takatifu inatarajiwa kuanza hapo saa 4:30 asubuhi kwa saa za Ulaya. Tukio hili limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Familia kwa kutambua wito na dhamana waliyo nayo wazee katika maisha ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia Rais wa Baraza la Kipapa la Familia anasema, lengo ni kutaka kuonesha umuhimu wa wazee katika jamii na kwamba, ni kundi linalohitaji kupendwa, kuthaminiwa na kutunzwa. Wazee wamekuwa mstari wa mbele katika dhamana ya kurithisha imani, tamaduni na mapokeo katika Jamii. Hii ndiyo kazi iliyoshuhudiwa na Wazee kama akina Anna wanaozungumziwa kwenye Maandakiko Matakatifu. Wazee ni kundi linaloshuhudia matumaini hata kwa vijana wa kizazi kipya!







All the contents on this site are copyrighted ©.