2014-07-01 08:42:17

Sifanyi maamuzi katika upweke!


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amefanyiwa mahojiano na Franca Giansoldati wa Gazeti linalochapishwa kila siku mjini Roma, lijulikanalo kama Il Messaggero kwa kusema kwamba, dhamana ya kimaadili inahitaji ujasiri na moyo mkuu. RealAudioMP3

Kwa ufupi ni kiini cha majibu ambayo Baba Mtakatifu ameyatoa alipokuwa akijibu maswali mbali mbali kuhusiana na changamoto zinazoikumba miji mikuu kama vile Roma; mabadiliko yanayodhohofisha sera na mikakati ya kiuchumi; umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi; maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; utu na heshima ya binadamu; utumwa mamboleo unaowatmbukiza hata watoto katika biashara ya ngono; kazi za suluba wanazofanyishwa watoto wadogo, kiasi cha kuathiri makuzi yao bila kusahau nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zinazofanywa na watu ambao wamepewa dhamana ya kuwalinda na kuwasimamia watoto wadogo.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, yeye ni mgeni sana mjini Roma kuna mambo mengi ambayo anaendelea kujifunza kwa mfano tangu azaliwe hakuwahi kuingia kwenye Kikanisa cha Sistina kilichoko mjini Vatican, eneo ambalo lina mvuto mkubwa kwa watalii kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lakini yeye ameingia humo kwa mara ya kwanza wakati wa uchaguzi wa Papa Benedikto XVI kunako mwaka 2005 na kwamba, hajawahi kutembelea kwenye Makumbusho ya Vatican yenye utajiri mkubwa wa sanaa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Analifahamu sana Kanisa la Bikira Maria mkuu kwani hapo mara nyingi alikwenda kusali. Amewahi kutoa huduma za kichungaji wakati alipokuwa Kardinali kwenye Kanisa la Mtakatifu Laurent. Anakiri kwamba, Piazza Navona anaifahamu kwani hapo kulikuwa na nyumba ya wageni aliyokuwa anaitumia kila wakati alipokuwa anafika Roma.

Katika miji mikuu anawakumbuka zaidi vijana na changamoto wanazokabiliana nazo mijini, ndiyo maana Mwezi Novemba 2014, kutafanyika Kongamano la shughuli za kichungaji kwenye miji mikuu litakaloadhimishwa Jimbo kuu la Barcellona. Miji mikuu inafumbata tamaduni za watu mbali mbali, lakini pia ina changamoto zake kwani huko kuna idadi kubwa ya wahamiaji na wageni wanaotafura ubora na usalama wa maisha. Kanisa halina budi kusoma alama za nyakati ili kuwasaidia wananchi wanaoishi mjini, ili waweze kuonja Injili ya Furaha.

Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya Mababa Watakatifu ambaye hakushiriki katika maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, lakini anatambua mchango mkubwa uliotolewa na Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI katika mchakato wa Uinjilishaji. Waraka wake wa Evangelii Nuntiandi ni dira na mwongozo kwa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.

Kwa watumishi wa Serikali, wanapaswa kwanza kabisa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu, zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu na kwamba, mwanasiasa anapaswa kujikita katika fadhila ya upendo. Tatizo kubwa linalojitokeza katika siasa ni: rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma.

Huduma kwa wananchi inapaswa kuwa ni msingi bora kwa wale wote wanaotaka kupewa fursa za kuongoza wananchi katika mchakato wa kujiletea maendeleo endelevu. Matatizo haya ya kijamii yamepembuliwa vyema sana katika Liturujia ya Neno la Mungu kwa siku za hivi karibuni na kwamba, amepata nafasi ya kuwashirikisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kile kilichomgusa katika Neno la Mungu.

Anasema mla rushwa na mpenda rushwa hana rafiki. Rushwa na ufisadi kwa sasa ni majanga ya kimataifa. Wanasiasa wengi waliofanya mabadiliko wamepelekea wakati mwingine kumong’onyoka kwa tunu msingi za kimaadili katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na katika vyombo vya fedha. Mtikisiko wa uchumi kimataifa ni matunda ya ubinafsi na rushwa!

Baba Mtakatifu anasema, anasikitishwa sana na umaskini wa hali na kipato na anakwazika zaidi na mmon’gonyoko wa maadili na utu wema; kwani haya ni mambo ambayo yanagusa utu na heshima ya binadamu. Biashara ya utumwa mamboleo; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni mambo yanayowaathiri vijana, lakini yanachochewa na watu wazima wenye uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka, watu waliofilisika kimaadili na kiutu. Sera makini za kijamii zinaweza kusaidia kukuza na kuboresha maadili na utu wema.

Kanisa halina budi kujielekeza zaidi na zaidi katika kuwajengea watu uwezo wa kupambana na changamoto za maisha kwa kukuza na kudumisha dhamiri nyofu. Waamini wapewe majiundo awali na endelevu kuhusu: Kanuni ya Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na maisha ya Sala, kwa ufupi waamini wajitahidi kuifahamu Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, ili kuimwilisha katika uhalisia wa maisha!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukumbatia Injili ya Uhai na kuachana kabisa na utamaduni wa kifo unaokumbatia sera za utoaji mimba. Watoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu wapokelewe na kutunzwa kwa heshima zote. Watu wasiwe ni watuma wa mali, madaraka na sifa. Mafundisho ya Heri za Mlimani ni muhtasari wa kanuni msingi za maisha ya Kikristo. Wanawake wanayo nafasi kubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kwani Kanisa linajitambulisha kuwa ni Mama na Mwalimu.

Baba Mtakatifu anasema, katika mikakati yake ya shughuli za kichungaji kwa sasa anapenda kujielekeza zaidi Barani Asia. Mwezi Agosti anatarajiwa kushiriki katika Kongamano la sita la Vijana wa Bara la Asia litakaloadhimishwa huko Korea ya Kusini.

Mwezi Januari anatarajiwa kwenda nchini Sri Lanka na Ufilippini, kwa hakika kuna matumaini makubwa kwa Kanisa Barani Asia. Nchini Korea, Kanisa linategemezwa na waamini walei, matendo makuu ya Mungu. Hapa kuna waamini ambao wamejisaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. China bado ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa sasa anatekeleza changamoto na maelekezo yaliyotolewa na Makardinali katika mikutano yao elekezi wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hana jipya analolifanya, bali ni mwendelezo wa maisha na utume wake hata kabla ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa. Hakuna jambo ambalo analifanya katika upweke, haya ni matunda ya uongozi shirikishi ndani ya Kanisa, kwa kukazia umuhimu wa Sinodi, ingawa ni dhana ambayo Makardinali wengi hawapendi kuisikia.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawashukuru waamini wa Jimbo kuu la Roma katika Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paul, waendelee kuonesha ujasiri na ushuhuda wa imani, daima wakiwa na furaha, matumaini na imani inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha kwa wakati huu!

Mahojiano haya yamehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.