Mara baada ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo iliyoadhimishwa
mjini Vatican na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 29 Juni 2014 na kuwavika
Maaskofu wakuu Palio Takatifu, Watanzania wanaosoma na kuishi mjini Roma walikusanyika
kwa hafla fupi, ili kumpongeza Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea.
Katika
nasaha zake kwa watanzania, Askofu mkuu Dallu amewataka watanzania kuombea umoja wa
nafsi unaojengwa katika upendo unaobubujika kutoka kwa Yesu Kristo; umoja wa taifa
la Tanzania unaopaswa kujengeka kutokana umoja wa nafsi, ili Tanzania iweze kuendelea
kuwa ni taifa linalojengeka kutokana na umoja wa nafsi na wala si vinginevyo; taifa
linalojikita katika umoja wa kitaifa kwa kukazia misingi mikuu inayowaunganisha watanzania
licha ya tofauti zao za kisiasa, kidini na kikabila.
Askofu mkuu Dallu amewataka
watanzania kutokubali kumegwa wala kugawinyika kwa misingi yoyote ile kwani makundi
ya namna hii yanaweza kukosa mwelekeo na dira katika ujenzi wa misingi ya umoja wa
kitaifa inayojika katika ukweli, upendo, haki na amani.
Naye Padri Dietrich
Canisius Pendawazima Kihaule, Makamu mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Consolata
katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema ameguswa sana na ujumbe uliotolewa
na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake, kwa kuwataka Maaskofu na waamini
wote kutokuwa na woga wa kuhubiri Injili, Kumtangaza na Kumshuhudia Yesu aliyeteswa,
akafa na kufufuka kutoka katika wafu.
Anasema, Yesu anawapatia wafuasi wake
nguvu na ujasiri wa kushinda woga na wasi wasi, ili kusonga mbele kwa ujasiri na matumaini
makubwa, kwa kutangaza na kuumwilisha upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa
lake. Anawahimiza waamini kuwa imara na hodari ili kumshuhudia Kristo katika maisha
ya kila siku!