2014-06-30 09:05:31

Waombeeni Mapadre wenu!


Mpendwa msikilizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kirsto. Leo tunapoadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mama Kanisa anatualika kusali kuombea utakaso wa Mapadre wetu kwani, katika Sherehe hii, imewekwa nia maalumu pia ya kuwatakatifuza mapadre. Tuungane pamoja kabisa kuwaombea mapadre wetu wapendwa. RealAudioMP3

Tuwaombee imani thabiti, ujasiri na uvumilivu, ili mwovu asiwaweze. Tuwaombe umoja, upendo na mshikamano katika kutuhudumia sisi kwa neno la Sakramenti. Zaidi ya hayo tuendelee kumshukuru Mungu kwa zawadi ya upadre katika kanisa na katika ulimwengu huu.

Mapadre wanatoka wapi? Kwa mwangwi wa Kitabu cha Waebrania (sura ya 5), hawa makuhani wametwaliwa kutoka kwa watu na kwa ajili ya watu, yaani, wametoka kwetu sisi wenyewe na kwa ajili ya wokovu wetu. Ili watende kazi yao vema, sisi waamini wote tunaalikwa, tuwape nafasi watutumikie vizuri, tuwape ushirikiano mwema, ushirikiano usio kikwazo, ili kwa ushirikiano huo wa kichungaji, Kanisa la mungu lisonge mbele, Mungu atukuzwe na sisi tuokolewe

Leo tunapomshukuru Mungu kwa zawadi ya Upadre na Mapadre katika Kanisa, tujikumbushe kidogo juu ya hadhi na thamani ya padre. Tusaidiwe na mawazao ya baadhi ya Watakatifu.

Mtakatifu Yohane Maria Vianey anasema, upadre ni Upendo wa moyo wa Yesu; na hivyo padre mwenyewe ni pendo la moyo wa Yesu. Upadre ni zawadi inayotoka ndani kabisa ya moyo wa Yesu, unaowaka moto wa mapendo ya kutaka kuwaokoa watu wote. Upadre ni upendo wa Yesu mwenyewe, unaoendeleza kazi ya ukombozi wa Roho za watu. Upadre ni chemchemi ya upendo wa moyo wa Mwokozi, ni kisima cha wokovu. Kwa maana hiyo basi, padre ni zawadi ya moyo wa Yesu kwa ulimwengu. Padre anaendeleza kazi ileile ya Yesu kwa ulimwengu.

Mababa wa Kanisa wanamtazaama Padre kuwa ni Kristo mwingine [Alter Christus], ni Yesu wa pili. Padre ni makao, ni maskani ya Yesu hapa duniani.

Mtakatifu Yohane wa Dameski, anafananisha utume wa Padre na utume wa Mama Bikira Maria; yaani, utume wa kumleta Yesu duniani kwa uweza na nguvu ya Roho Mtakatifu. Padre anafanya Kazi ya kumleta Mungu duniani kwa njia ya huduma ya NENO na adhimisho takatifu la ALTARENI. Jinsi Bikira Maria alivyomleta mwokozi katika historia, Padre anamleta Kristo katika NENO na SAKRAMENTI. Hivyo, Padre anafanya kazi ya kuleta wokovu duniani, anapoadhimisha mafumbo matakatifu. Hapo anatangaza na kupeleka upendo, huruma, furaha, msamaha, mwanga, neema, baraka na uzima wa milele kwa watu.

Mtakatifu Agustino anafanaifananisha mikono ya Padre iliyopakwa mafuta na tumbo la Bikira Maria ambalo kwalo NENO wa Mungu alitwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatatifu akakaa kwetu. Kwa Mikono ya Padre na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Bwana wetu Yesu Kristo anatwaa mwili altareni na anakaa kwetu katika Ekaristi.

Upadre ni upendo wa Moyo Mtakatifu wa Yesu (Hili ni fundisho la Mtakatifu Yohane Marie Vianney). Daraja Takatifu la Upadre lina hadhi na thamani kubwa sana, ndiyo maana Mtakatifu Yohane Maria Vianney Msimamizi wa Mapadre wote anasema kuwa Upadre ni Upendo wa Moyo wa Yesu. Jinsi Upendo wa Moyo wa Yesu ulivyo na Hadhi na Thamani kubwa sana kwa Mwanadamu, ndivyo na Upadre ulivyo wa Thamani kubwa.

Padre ana thamani ya Moyo wa Yesu. Padre ana hadhi na thamani ya ki – Mungu. Ndiyo maana Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alijua kuwa Mapadre ni Malaika na aliwapenda sana kwa sababu kwake kuwa na Padre ni kuwa na YESU mwenyewe. Kwa sababu Padre anagawa mafumbo yaleyale ya Upendo wa Yesu. Anaendeleza kazi ya Ukombozi hapa Duniani.


Kutokana na Hadhi na Thamani kubwa aliyonayo Padre ndiyo maana Mt. Fransisko wa Assisi alisema: “kama nikikutana na Padre wako wawili na Malaika, kwanza nitamsalimu Padre niibusu na mikono yake iliyotiwa mafuta, mikono inayomshusha Yesu katika sadaka ya altare. Malaika ni rafiki wa Mungu, lakini Padre anashika nafasi ya Mungu hapa Duniani”.

Padre ni zawadi ya ajabu ya Upendo wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Zawadi yenye uweza na nguvu za Mungu. Mapadre wetu wana nguvu ya pekee ya kuondolea Dhambi. Wana Nguvu ya kushusha na kugawa Mwili wa Damu Takatifu ya Yesu. Nguvu ya kuadhimisha Masakramenti. Nguvu ya kutubariki sisi na kubariki vitu, wana nguvu ya pekee ya kuendeleza kazi ya ukombozi duniani.

Ni kwa njia hiyo mapadre wetu, wana nguvu ya kuwa watetezi wa Wanyonge. Padre ni Sura ya Upendo wa Moyo wa Yesu kwa Watu wote. Padre ni Baba wa Upendo kwa watu wote. Mapadre wetu, pamoja na nguvu zote za kikuhani, wana nguvu ya pekee pia ya Kinabii, inayowazesha kutangaza mapenzi ya mungu, kukaripia maovu na kuwatia moyo waliopondeka roho.

Padre anatoa wapi nguvu hizo? Padre amepewa na Yesu Mwenyewe mamlaka ya kutumia uweza wake. Mamlaka na uweza kwa ajili ya Utume na Huduma ya Upendo. Ndiyo maana mababa wa Kanisa wanasema, Padre hutenda katika nafsi ya kristo na kwa jina la kanisa. Yote mawili yanakwenda pamoja. Padre anafanya kazi kwa nguvu ya Mungu. Nguvu hiyo ni kwa ajili ya Diakonia (Utumishi), kwa ajili ya Uchungaji na kwa ajili ya uangalizi na wokovu wa roho zetu.

Padre amepewa mamlaka ya kutumia Nguvu za Mungu na Bwana Yesu. Padre amepewa Nguvu za moyo wa Yesu. Uweza wa Mungu unafanya kazi ndani ya Padre. Upendo wa Moyo wa Yesu unafanya kazi ndani ya Padre. Bwana Yesu anawasha moto wa Upendo wa Moyo wake Mtakatifu ndani ya Padre. Karama na vipaji vyote vya Upendo wa Moyo wa Yesu, vimo ndani ya Padre kwa ajili ya wokovu wa watu na kwa ajili ya sifa na Utukufu wa Mungu.

Mpendwa msikilizaji, tunapomshukuru Mungu kwa zawadi ya Mapadre katika Kanisa, tuendelee kuwaombea sana ili shetani asiwaangushe. Afadhali kuwaombea mapadre kuliko kushika projekt ya kuwasemasema na kuwasumbua hovyo, unawaongezea ugumu wa kazi. Mapadre wetu wanaomba na wanahitaji sana sala zetu ziwasaidie. Mt. Yohane Maria Vianey anasema, Padre ni adui mkubwa sana wa shetani. Ndiyo maana shetani hapendi mapadre kabisaa!! Kwa Padre anapoungamisha watu nao wakiondolewa dhambi zao, ni kama shetani ananyanganywa wateja wake. Ndiyo maana daima Mapadre wetu wanapata mashambulizi makubwa na mabaya mno!!. Wapo watu wengi sana kwa hila za shetani wanapenda kuwaangusha mapadre. Na shetani anajua anachofanya “Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika”. Katika mradi wa shetani wa kulishambulia Kanisa, anaelekeza mizinga yake kwa Mapadre wetu, ambao ndiyo wachungaji wa roho zetu.

Tunapowashukuru na kuwaombea Mapadre wetu, papo hapo tusisahau kuombea miito ya Upadre, Utawa na Ukatekista katika Kanisa. Tuwalee watoto wetu katika imani, elimu na maadili, ili waisikie na waiitikie sauti ya Mungu inayowaita, siku moja nao wasimame altareni, wazinene siri za Kristo na kutugawia mafumbo ya wokovu. Kanisa linahitaji watendakazi kwani mavuno ni mengi na watendakazi ni wachache.

Tukiongozwa na neno lisemalo “Wakumbukeni viongozi wenu waliowahubirieni neno la Mungu, Fikirini juu ya mwenendo wao, mkaiige imani yao” (Ebr.13:7), tunapomshukuru Mungu kwa zawadi ya upadre na mapadre wetu, tuwaombee huruma ya Mungu mapadre wetu wote waliotangulia mbele za kiti cha haki. Bwana mwenye huruma, apokee sadaka ya kazi zao, jasho lao, machozi yao, na hata damu yao, awapanguse jasho la kazi yao ya hapa duniani, awastahilishe kushiriki mafumbo ya milele huko Mbinguni. Amina.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.