Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican anawataka waamini kuonesha ujasiri na ari kwa kumshuhudia
Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kwa njia
ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Anawashukuru
waamini ambao daima wamekuwa mstari wa mbele katika kujisadaka kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya jirani zao.
Askofu mkuu
Mamberti ameyasema haya hivi karibuni katika maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu
kwa ajili ya wanachama wa Chama cha Watakatifu Petro na Paulo pamoja na kupokea ahadi
kwa wanachama wapya waliojiunga na Chama hiki, kwa kuwataka kuendelea kuwa waaminifu
kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya huduma.
Askofu mkuu Mamberti anawataka
wanachama kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu na kwa njia hii watakuwa
na ujasiri wa kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha kumshuhudia
kati ya watu. Hapa mambo mawili yanakwenda sambamba, yaani imani na uaminifu kwa Mungu
kama msingi wa huduma makini inayotolewa na wanachama hawa kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii, ili kujenga na kuimarisha Kanisa la Kristo.
Askofu mkuu
Mamberti anawaalika wanachama hao kuwashirikisha hata vijana katika mchakato wa huduma
kwa maskini, ili kuendeleza utume huu hata kwa siku za usoni, kwani ni huduma inayojielekeza
zaidi katika maisha ya kiroho na kitamaduni. Watambue kwamba, Baba Mtakatifu anathamini
sana mchango na huduma wanayoitoa kwa niaba ya Kanisa, katika unyoofu, ukarimu na
sadaka ya mambo mengi katika maisha.
Askofu mkuu Mamberti anawashukuru wanachama
hawa kwa mapokezi mazuri wanayoyafanya kwa waamini na mahujaji wanaomiminika kila
siku kusali na kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican; kwa kusimamia
na kuratibu ibada zinazoadhimishwa ndani ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro bila kusahau
huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Huu wote ni ushuhuda
wa huduma ya mapendo kwa Kristo na Kanisa lake.
Askofu mkuu Mamberti anawataka
wanachama hao kuendeleza moyo wa upendo na ukarimu kwa watu wanaokutana nao katika
huduma, ili waweze kubaki na picha yenye kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa
wote wanaomtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Hii ni huduma inayowataka kuonesha
ukarimu wa pekee, uvumilivu na heshima kwa watu, weledi, lakini zaidi, ushuhuda wa
imani, matumaini na mapendo yanayomwilishwa katika matendo.
Baada ya maadhimisho
ya Ibada ya Misa takatifu, baadhi ya wanachama wamepewa tuzo ya heshima kutokana na
kujipambanua zaidi katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa
Jamii.