2014-06-30 09:41:02

Nimewaombea!


Askofu mkuu Damian Dallu wa Jimbo kuu la Songea, Tanzania ni kati ya Maaskofu wakuu 27 waliovikwa Pallio Takatifu wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, mitume, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 29 Juni 2014. RealAudioMP3

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Dallu anamshukuru Mwenyezi Mungu, Baba Mtakatifu Francisko, Kanisa la Tanzania na kwa namna ya pekee Jimbo kuu la Songea. Anasema amepata fursa ya kuiombea Familia ya Mungu katika ujumla wake wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Wakatifu Petro na Paulo mitume na kwamba, anamshukuru Mungu kwa wema na baraka zake anazolikirimia Kanisa.

Anasema, kwa maombezi ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, waamini wajitahidi kuwa kweli ni mashahidi wa imani, kwa kujitoa bila ya kujibakiza. Ametumia fursa hii pia kuliombea Taifa la Tanzania ili liweze kuendelea kustawi katika upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya kumtukuza Mungu, ili kwamba, umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania uweze kuzaa matunda ya umoja wa mataifa yote.

Naye Padre Alcuin Nyirenda, OSB katika mahojiano na Radio Vatican amegusia historia fupi ya Pallio Takatifu wanayovishwa Maaskofu wakuu kama alama ya mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, changamoto na mwaliko kwa Maaskofu wakuu kuwa kweli ni Wachungaji wema wanaoweza kuthubutu kujisadaka kwa ajili ya kuwatafuta Kondoo waliopotea. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, Pallio Takatifu ilitolewa na Papa Gregory Mkuu alipomtuma Askofu mkuu Augustino wa Cantebury kwenda Uingereza kwa ajili ya kuinjilisha.

Ni katika mantiki hii kwamba, Askofu mkuu Damian Dennis Dallu wa Jimbo kuu la Songea kama mmissionari anatumwa na Mama Kanisa kuwaitangazia Familia ya Mungu Jimbo kuu la Songea Injili ya Furaha na Matumaini. Anatumwa kutangaza na kulishuhudia Neno la Mungu, ili kweli Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Songea, liweze kujipambanua kuwa ni Kanisa la Kristo linalosimikwa katika misingi ya umoja, upendo na mshikamano kama Jumuiya ya Waamini.







All the contents on this site are copyrighted ©.