Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Askofu
wa Jimbo Katoliki la Iringa, tarehe 1 Julai 2014 anasherehekea kilele cha Jubilee
ya miaka 25 ya Uaskofu. Itakumbukwa kwamba, Askofu Ngalalekumtwa alizaliwa tarehe
25 Oktoba 1948 huko Iringa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa
tarehe 17 Aprili 1973.
Tarehe 14 Novemba 1988 akateuliwa na Mtakatifu Yohane
Paulo II kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo Katoliki Sumbawanga. Tarehe 6 Januari 1989
akawekwa wakfu kuwa Askofu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na Papa
Yohane Paulo II. Tarehe 21 Novemba 1992 akateuliwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki
Iringa.
Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Ngalalekumtwa anasema,
Mwenyezi Mungu amempatia fursa katika kipindi cha miaka 25 kuwafundisha, kuwatakasa
na kuwaongoza watu wa Mungu katika njia za haki na uadilifu katika Bwana. Amejitahidi
kutumia muda, nguvu na vipaji vyake kwa ajili ya ustawi wa Kanisa na maendeleo ya
binadamu.
Anasema furaha kubwa kwa mchungaji ni pale anapojituma bila ya kujibakiza
kwa ajili ya watu wake; ni ile hali ya kushiriki katika furaha na machungu ya watu
wake kwa kutambua kwamba, hata yeye ni sehemu ya Familia ya Mungu. Katika maisha amekabiliana
na changamoto nyingi kama vile uchovu, magumu ya maisha, vipindi vya majaribu kwa
mtu binafsi, kwa Kanisa na Jamii husika. Katika hali kama hii kunahitajika utulivu,
sala na maombi kutoka kwa watu mbali mbali.
Jubilee ya miaka 25 ya Uaskofu
ni kipindi cha kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na yote aliyomwezesha kutekeleza
katika kipindi chote hiki. Jubilee ni kipindi cha kuomb toba na msamaha kwa mapungufu
ya kibinadamu, kwani Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, mapendo na msamehevu. Anamwomba
Mungu amzidishie neema na baraka pale alipofanya vyema, amhurumie pale alipomsaliti.