2014-06-29 08:55:08

Sanaa ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya Kiekumene


Katika mkesha wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Jumamosi tarehe 28 Juni 2014, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali wameshiriki katika tamasha la nyimbo za dini lililoongozwa na Kwaya kutoka Upatriaki wa Mosco na kwaya ya Kikanisa cha Sistina, kama sehemu ya mchakato wa kukoleza majadiliano ya kiekumene kwa njia ya nyimbo. Kwaya hizi mbili pia zimeshirikiana kwa pamoja katika Ibada ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 29 Juni 2014.

Kardinali Parolin amewashukuru wafadhili na wadau mbali mbali kwa kuwezesha kwaya hizi mashuhuri kutumbuiza na kwa namna ya pekee, ametoa shukrani zake za dhati kwa Patriaki Kirill na kwa Kanisa zima la Kiorthodox la Moscow, kwa kufanikisha tukio hili ambalo ni mwendelezo wa hija ya pamoja kati ya Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki, ili kushirikishana uzoefu na mang'amuzi kwa kulenga umoja kamili kati ya Wakristo.

Kuna uhusiano wa karibu sana na Fumbo la Mungu kwa wale wanaotafuta kilicho kweli, chema na kitakatifu. Kwa wasanii wa Kikristo wanaojisadaka kwa kusukumwa na imani watambue kwamba, wanatekeleza utume wao wa Kikanisa kwa ajili ya huduma kwa utukufu wa Mungu na mng'ao wa sura ya Kristo. Kuna tofauti kubwa ya mapokeo ya muziki mtakatifu kati ya Kwaya hizi mbili, lakini zote kwa pamoja zimewawezesha kuonjesha uzuri wa kukutana mbele ya Mkombozi.

Kardinali Parorin anasema, sanaa pia inapaswa kuwa ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa ya Mashariki na Makanisa ya Magharibi, ili kwa pamoja waweze kuchangia utajiri huu kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, kwa kukuza na kutukuza kazi ya uumbaji, madhara ya dhambi sanjari na ukombozi wa mwanadamu.

Muziki mtakatifu unafumbatwa pia katika Fumbo la neema ya Mungu inayowahamasisha Wakristo kutafuta umoja kamili. Ushiriki wa kwaya hizi mbili katika Ibada ya Misa Takatifu katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani ni kielelezo makini cha ile hamu ya umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo. Hii ni kiu ya kutaka kutembea kwa pamoja, kwa kushirikiana kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba, waendelee kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Kanisa kadiri ya mapenzi ya Kristo mwenyewe.







All the contents on this site are copyrighted ©.