2014-06-29 14:36:37

Neema na huruma ya Mungu inavyotenda maajabu!


Tangu wakati wa Kanisa la Mwanzo, Kanisa la Roma kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni linaadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo; Mitume ambao wamefanywa kuwa ndugu kwa njia ya imani kwa Yesu Kristo na kifo dini kiasi kwamba, wamekuwa wamoja katika Kristo Yesu. Hata katika utoafuti wao wa kibinadamu na karama walizojaliwa na Mwenyezi Mungu, wamechaguliwa na wakajibu wito huu wa kuyasadaka maisha yao!

Kwa njia ya neema na baraka za Kristo wamegeuzwa na kuwezeshwa kutenda makuu katika maisha na utume wao. Simoni Petro aliyemkana Yesu mara tatu wakati wa mateso yake na Saulo ambaye alilidhulumu Kanisa la Kristo, wamebadilika na kuukumbatia upendo na huruma ya Mungu, kiasi kwamba, wamebarikiwa kuwa kweli ni Marafiki na Mitume wa Yesu. Hata leo hii wanaendelea kuzungumza na kulionesha Kanisa dira na mwongozo wa kufuata!

Ni tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 29 Juni 2014 wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Ni watakatifu wanaolihamasiaha Kanisa kuonesha ushuhuda wa maisha kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kwa kuwashirikisha na kuwaonjesha nguvu inayobubujika kutoka kwa Yesu Kristo. Kanisa linatambua kwamba, halina fedha wala dhahabu lakini linaweza kutenda miujiza kwa nguvu ya Yesu Kristo, kwa kuwaponya na kuwaganga wale waliopondeka mioyo.

Mtakatifu Paulo, Mwalimu wa Mataifa alitokewa na Yesu Mfufuka akiwa njiani kwenda Damasko kulidhulumu Kanisa hapa akabadilika na kuwa mtu mpya kabisa, kwanza alikuwa ni mtesi na adui mkubwa wa Kanisa, lakini anapotubu na kuongoka anakuwa ni mtu anayejisadaka kwa ajili ya huduma ya Injili. Neno la Mungu lilete mabadiliko katika maisha ya watu, kwa kushinda ubinafsi na kuanza kumfuasa Yesu, Bwana na Mwalimu aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya rafiki zake.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Sherehe hii ni changamoto kubwa kwa waamini kuona huruma ya Mungu inavyotenda kazi katika maisha ya Watakatifu Petro na Paulo.

Mwenyezi Mungu anapenda kuwakirimia waamini neema zake kama alivyofanya kwa Watakatifu Petro na Paulo. Bikira Maria awasaidie waamini wakati wa majaribu na awezeshe kuwa na nguvu ya kumshuhudia Kristo na Injili yake. Baba Mtakatifu anawaombea kwa namna ya pekee Maaskofu wakuu wapya walioteliwa hivi karibuni ambao wamevishwa Pallio Takatifu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.