Baba Mtakatifu Francisko katika sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani,
Jumapili tarehe 29 Juni 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Pallio Takatifu
kwa Maaskofu wakuu ishirini na saba, kati yao sita kutoka Barani Afrika na Maaskofu
wakuu watatu hawakuweza kuhudhuria Ibada hii, kwa hiyo, Pallio zao watapewa na Mabalozi
wa Vatican katika nchi husika.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ametambua
uwepo wa ujumbe wa kiekumene kutoka kwa Patriaki Bartholomeo wa kwanza katika Ibada
hii ulioongozwa na Askofu mkuu Ioannis kama sehemu ya mchakato wa kuendelea kuimarisha
hija ya kidugu kati ya Wakristo ili hatimaye, kuweza kufikia lengo la umoja kamili,
hamu ya Makanisa haya mawili.
Baba anasema, Mtakatifu Petro alipoanza utume
wake kwenye Kanisa la mwanzo mjini Yerusalemu kulikuwa na wasi wasi na woga kutokana
na madhulumu ya Mfalme Erode dhidi ya Kanisa. Aliwafurahisha wananchi kwa mauaji ya
Mtume Yakobo na baadaye alimtupa gerezani Mtakatifu Petro, lakini akaokolewa na mkono
wa Malaika, matendo makuu ya Mungu na kwamba, Mungu anaweza kuwaokoa waja wake kutoka
katika woga na wasi wasi na kila aina ya minyororo, ili kuwaweka kweli huru, hiki
ndicho kiini cha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo anasema Baba Mtakatifu.
Baba
Mtakatifu anawauliza Maaskofu wenzake, Je, wanaogopa nini katika maisha na shughuli
zao za kichungaji? Ni wapi wanapokimbilia ili kupata faraja na usalama wa maisha yao?
Je, wanapata hifadhi kwa wakuu wa dunia na watu wenye mamlaka? Je, wanamezwa na kiburi
pamoja na mafanikio wanayopata, kiasi cha kuwafanya kujisikia kuwa huru zaidi? Baba
Mtakatifu anawauliza Maaskofu, Je, ni wapi wanapokita usalama wao?
Ushuhuda
wa Mtakatifu Petro unawakumbusha kwamba, imani kwa Mwenyezi Mungu ndilo kimbilio lao
la kweli, kwani ana nguvu ya kuwaondolea woga na kuwaweka huru kweli kutoka katika
utumwa na vishawishi vya dunia hii. Maaskofu wakuu na wale waliovikwa Pallio Takatifu
wanahamasishwa kufuata mfano bora wa maisha kutoka kwa Mtakatifu Petro sanjari na
kuhakiki imani yao kwa Mwenyezi Mungu.
Mtakatifu Petro baada ya kuulizwa mara
tatu na Yesu, ikiwa kama kweli alikuwa anampenda, anaambiwa kuchunga na kulisha Kondoo
wa Yesu. Hapa Mtakatifu Petro aliweza kuungama hadharani upendo wake kwa Kristo mara
tatu na hivyo kurekebisha kile kitendo cha Mtakatifu Petro kumkana Yesu mara tatu
wakati alipokuwa anasulubiwa. Tukio hili liliacha madonda makubwa katika moyo wa Mtakatifu
Petro, wakati huu, Petro anatambua mapungufu yake ya kibinadamu na kujiachilia ili
kuongozwa na huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani na hapa woga, wasi wasi
na ukosefu wa usalama vinatoweka mara moja.
Mtakatifu Petro anang'amua kwamba
uaminifu wa Mungu ni mkubwa zaidi kuliko mapungufu yake ya kibinadamu yaliyompelekea
hata akamkana Yesu mara tatu. Uaminifu wa Mungu unafukuzia mbali wasi wasi na uwezo
wa mwanadamu kufikiri. Hata leo hii, Yesu anaendelea kuwauliza wafuasi wake, Je, mnanipenda?
Lengo ni kung'amua wasi wasi na magumu ya maisha wanayokabiliana nayo kila siku, ili
kuweza kujiachilia mikononi mwa Mungu anayefahamu yote na kujiaminisha kwake Yeye
ambaye ni mwaminifu daima na kamwe hawezi kuwaacha kamwe!
Baba Mtakatifu anasema,
uaminifu wa Mungu unawaimarisha Wachungaji kinyume kabisa cha uwezo, imani na huduma
kwa Mungu na jirani katika upendo. Upendo unaobubujika kutoka kwa Yesu unamtosha Mtakatifu
Petro na wala hana sababu ya kuwa na wivu usiokuwa na mashiko, bali kupiga moyo konde
na kumfuasa Kristo kwa ari na ujasiri mkuu zaidi. Mang'amuzi haya ya Mtakatifu Petro
ni muhimu sana hata kwa Maaskofu wakuu leo hii!
Yesu leo hii anaendelea kuwaita
wote kumfuasa, hakuna sababu ya kupoteza muda kwa udadisi usiokuwa na mashiko, au
kwa kushikamana na mambo mpito na badala yake kujikita katika mambo msingi na kumfuasa
Yesu, licha ya magumu na changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza katika maisha
na utume wao. Wanaitwa kumfuasa Yesu kwa njia ya kuhubiri, kushuhudia kwa maisha ya
neema inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo na Daraja Takatifu, kumnadi
Yesu katika vipaumbele, uhalisia na majadiliano ya maisha.
Wanaitwa kumfuasa
Yesu katika mchakato wa utangazaji wa Injili ya Furaha hasa kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii, ili kwamba, asiwepo hata mtu mmoja anayekosa Neno la uzima linalomkomba
mwanadamu kutoka katika woga kwa kumkirimia uaminifu kwa Mwenyezi Mungu.