2014-06-28 07:42:48

Waonjesheni wagonjwa upendo na uaminifu wa Kristo!


Baba Mtakatifu Francisko kutokana na kuyumba kwa afya yake, Ijumaa jioni, tarehe 27 Juni 2014 dakika za mwisho alilazimika kuairisha hija yake ya kutembelea, kuzungumza na kusali pamoja na wagonjwa, wafanyakazi na wanafunzi wa Hospitali ya Gemelli, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa kitivo cha Tiba na Upasuaji cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ibada ya Misa takatifu imeongozwa na Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano ambaye pia ni Rais wa Taasisi ya Toniolo.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yaliyosomwa na Kardinali Scola anasema kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake na kwamba, upendo wake kwa binadamu hauna mipaka, ndiyo maana alifanya Agano la Mababa wa Imani, hata pale mwanadamu alipokengeuka na kupotoka katika Agano, Mwenyezi Mungu ameendelea kuwa ni mwaminifu katika ahadi zake.

Upendo na uaminifu wa Mungu vinapata ukamilifu wake katika maisha ya Yesu Kristo aliyejinyenyekesha hata kufa Msalabani, akaonesha uaminifu kwa Baba yake wa mbinguni na daima yuko tayari kumwonjesha mwanadamu upendo, huruma na msamaha wa dhambi zake, pale anapomkimbilia kwa moyo wa toba.

Upendo na uaminifu wa Mwenyezi Mungu unajionesha kwa namna ya pekee katika unyenyekevu wa Moyo wa Yesu ambaye amekuja hapa duniani ili kumwonjesha mwanadamu upendo unaobubujika kutoka katika hali ya unyenyekevu, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwa Yesu kwani Yeye ni mwenye Moyo mpole na mnyenyekevu. Hiki ndicho kiini cha Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambayo imeadhimishwa na Mama Kanisa, Ijumaa tarehe 27 Juni 2014 sanjari na Siku ya kuombea Utakatifu wa Mapadre.

Yesu Kristo anaonesha na kuwakirimia watu wote huruma ya Mungu, kiasi kwamba, waamini wanaweza kuonja upendo huu katika hatua mbali mbali za maisha yao: wakati wa furaha au wakati wa majonzi; wanapokuwa na afya au pale ambapo ni wagonjwa na hawajiwezi kitandani. Uaminifu wa Mungu ni fundisho kwa binadamu kupokea na kukumbatia zawadi ya maisha kama chimbuko la upendo wake, ili hatimaye, kuutolea ushuhuda kwa njia ya huduma makini inayofumbatwa katika hali ya unyenyekevu.

Hii ndiyo changamoto ambayo waganga na wahudumu wa sekta ya afya wanaalikwa kuimwilisha katika huduma kwa wagonjwa katika Hospitali ya Gemelli ambayo ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hapa kila mtu anajitahidi kuwaonjesha wagonjwa chembechembe ya upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kuzingatia weledi na umakini wa kazi.

Hii ina maana ya kukumbatia na kuwa waaminifu katika tunu msingi ambazo zilibainishwa na Padre Agostino Gemelli kwa taasisi za Kikatoliki nchini Italia, kwa kuunganisha tafiti zinazoangaziwa na mwanga wa imani ili kuwafunda watalaam wa Kikristo! Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, kwa kutafakari uaminifu wa Mungu, kila neno na tendo la Yesu linakuwa ni kielelezo cha upendo unaojikita katika huruma na uaminifu kwa Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya tafakari ya kina ili kuangalia kuhusu mahusiano yao na jirani zao na ikiwa kama wameendelea kuwa ni waaminifu, au wamekengeuka na kusambaratika kwa kufuata vionjo na hali zao za maisha? Haya ni majibu yanayoweza kutolewa na kila mwamini kwa kusukumwa na dhamiri yake nyofu na hatimaye, kumwomba Yesu ili awasaidie kufanana na Moyo wake Mtakatifu unaosheheni upendo na uaminifu!







All the contents on this site are copyrighted ©.