Umuhimu wa mchakato wa upatanisho na utulivu wa kisiasa!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi asubuhi, tarehe 28 Juni 2014 amekutana na kuzungumza
na Rais Hery Martial Rajaonarimampianina wa Jamhuri ya Watu wa Madagascar pamoja na
ujumbe wake, ambaye baadaye amekutana na kuzungumza pamoja na Kardinali Pietro Parolin,
Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Monsinyo Antoine Camilleri, katibu
mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Viongozi
hawa wawili wamepongeza uhusiano mwema uliopo kati ya pande hizi mbili na wamekazia
kwa namna ya pekee mabadiliko yanayoendelea kufanyika nchini Madagascar, pamoja na
kuangalia mchango wa Kanisa katika mchakato wa upatanisho wa kitaifa na utulivu wa
kisiasa. Wamelipongeza Kanisa kwa kuchangia katika maendeleo ya sekta ya elimu na
afya.
Baadaye, Baba Mtakatifu na mgeni wake wamejadili masuala mbali mbali
hasa kuhusiana na mapambano dhidi ya baa la umaskini na ukosefu wa usawa kijamii.
Wamegusia pia hali ya kimataifa hasa kutokana na kinzani za kivita na kijamii zinazoendelea
kugusa maisha ya watu.