2014-06-28 06:58:19

Sipati picha!


Tumezoea kusikia kuwa jumuia ya wakristu wa Kanisa la mwanzo walikuwa wanakaa pamoja na kushirikiana vizuri: “Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja.” (Mdo 4:32). Lakini kumbe kulikuwa pia na mivutano na migongano, mipinzani na kupishana katika fikra za watu.

Katika Kanisa la wakristu wa kwanza kulikuwa na makundi mawili yaliyokuwa daima yanapishana katika fikra. Kundi mojawapo ni lile la Wayahudi walioongokea ukristu (wakristu-wayahudi). Hao walikuwa wanashikilia zaidi mapokeo ya kiyahudi kadiri ya Agano la Kale, yaliyokuwa andalizi tu ya kumpokea Masiha Kristu aliyeishafika tayari.

Halafu kulikuwa na wakristu wengine walioyatambua mapokeo ya Agano la Kale na wakijua kwamba hatima yake ni Kristu, lakini walimfuata zaidi huyu Kristu siyo kung’ang’ania kushikilia mapokeo ya Agano la kale. Kwa hiyo tofauti hizo katika fikra zilikuwa kati ya wanamapokeo waliozingatia mila na desturi za asili hata zisizowezekanika bila kusoma ishara za nyakati; na fikra za wanamapinduzi wanaoongozwa na roho ya kweli ya mwanzilishi. Roho inayofungua akili ya kusoma ishara za nyakati na kuwawezesha kusonga mbele kwenye upya wa mambo.

Leo tunawashangilia kwa pamoja watakatifu Petro na Paulo. Mitume hawa mwanzoni walikuwa wanapishana katika fikra zao. Mathalani mtume Petro, alianza kufuata mapokeo ya Agano la kale, akishikilia mila na desturi za kiyahudi pamoja na zile za kikristu, kiasi cha kuwaudhi wengi katika kanisa la awali. Paulo, kumbe, alikuwa ni mwana mapokeo wa aina ya waamini wenye misimamo mikali ya kiimani, kutokana na mazingira aliyokulia na malezi ya awali aliyoyapata toka majalimu wa kifarisayo akawa mkereketwa sana wa dini ya kiyahudi. Toka huko akaongoka ghafla na kuwa mfuasi wa Yesu. Unaweza kupata picha ya aina hii ya walokole wa dini fulani, wakiongokea dini nyingine wanavyoendelea na ukereketwa katika dini waliyoongokea. Hawaambiliki!

Paulo alikuwa mlokole wa aina hiyo asiye na mzaha katika kumfuata Kristu. Unadhihirisha ukweli huu Antiokia, anavyomdharau na kushindana na Petro kadamnasi na kumwita mnafiki. “Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso. Kwa maana kabla hawajaja watu kadha wa kadha waliotoka kwa Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini walipokuja wao, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa. Na hao Wayahaudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata na Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao.” (Gal 2:11-13).

Bahati nzuri malumbano yao hayakuendelea, kwani Petro akaja kumwita Paulo kuwa ndugu yake mpenzi. “Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa.” (II Petro 3: 15). Hatimaye mitume wote wawili wametoa maisha yao kwa ajili ya Kristu na leo tunasherekea sikukuu yao. Baada ya kuona tofauti za fikra za mitume hawa wawili, sasa tuiangalie Injili ya leo inavyoweza kutusaidia kusoma ishara za nyakati na kuishi imani, licha ya tofauti za fikra zetu.

Tupo kaskazini ya Uyahudi, mahali paitwapo Kaisaria Filipo. Sehemu hii inasifika sana kwa rutuba, na kwa wingi wa maji ya chemchemi za mto Yordani na malisho mazuri ya mifugo. Alessandro mkuu alipofika hapo alipagawazwa sana na utajiri wa huluka akapaona kuwa ni Paradisi ya miungu wa rutuba, “Pan na Nimfe”. Akapabatiza jina “Paniass au Baniasi (mungu Pan wa kigiriki). Kadiri ya fikra za wakazi wa hapo, yaonekana mungu Pani alikidhi mahitaji ya watu kwa kuwapa rutuba kwa mazao, maji na malisho kwa wanyama wao.

Naye mfalme Filipo mtoto wa Herode, aliujenga mji mkuu pahala hapo kwa heshima ya Kaisaria Tiberius. Ili kuutofautisha na miji mingine ya Kaisari akauita Kaisaria Filipi. Akajenga pia hapo majengo mawili ya ghorofa na jengo mojawapo la roshani linaloonesha mandhali ya nchi na chemchemi ile nzuri. Filipo aliwapa raia maisha mazuri, pamoja na burudani. Mathalani, wakati wa sikukuu alikuwa anamwalika Salome, mdada mmoja gwiji wa kuimba na kucheza.

Dada huyu ndiye yule aliyecheza kule Makeronte mbele ya Herode, na kuzawadiwa kichwa cha Yohane Mbatizaji. Dada huyu alikuja baadaye kuolewa na Filipo mwenyewe. Kwa hiyo michango hii miwili ya mungu Pan nimfe, na mchango wa mfalme Filipo kwa taifa ni changamoto kubwa sana katika maisha ya watu. Yesu akiwa katika mandhali kama hii nzuri ya kijiografia na ya mchango mzuri wa mfalme Filipo katika kuboresha maisha ya raia, anawasaili mitume wake maswali mawili akiwataka wajihoji kwa dhati uchaguzi wa maisha yao. “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” (Mt. 16:13).

Ikizingatiwa pia kuwa mitume walikuwa wamerudi karibuni tu toka uchungaji, walikosikia jinsi watu walivyokuwa wanaongea na mategemeo yao toka kwa Yesu. Hapa unaona jinsi Yesu anavyoweza kusoma “ishara za nyakati,” jinsi watu wa wakati wake wanavyowaza na kutekwa na mambo yanayoweza kuwazuga na kuwasahaulisha na mambo makuu ya maisha.

Jibu la kwanza la mitume linaonesha kuwa Yesu hana jipya. Mchango wake unalingana tu na ule wa manabii wengine waliomtangulia. “Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.” (Mt 16:14). Manabii hao waliokuwa watu wa pekee, walioheshimika kutokana na mchango waliotoa wa hekima zao, miongozo yao, sera zao zilizoiongoza jamii katika njia ya haki.

Kwa vyovyote walimkiri Yesu kuwa ni mtu wa pekee, mtu bora, mahili, mwaminifu, mhubiri wa upendo, mtu wa amani lakini ni kama mmojawapo tu kati ya wengi. Mtazamo huo kwa Yesu unauona hadi leo, ambapo watu wa imani nyingine isiyo ya kikristu wanamwona Yesu kuwa ni wa pekee, nabii, kuhani, mwema, lakini ni mmojawapo tu kati ya watu maarufu “Yesu ni Nabii Isa kama walivyokuwa manabii wengine wakuu.”

Swali la pili ni muhimu zaidi kwani linadai kujihoji msimamo wako binafsi mbele ya wakuu hao wote, na mbele ya ulimwengu unaokuzunguka aidha swali linadai kuwa na ujuzi wa kusoma ishara za nyakati: “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” Waswahili wangesema “mimi ni mnani wenu?” Ni sawa na kusema: “Katika mambo yote ya ulimwengu huu, mimi ninayo nafasi gani katika maisha yako binafsi?”

Petro anajitosa kujibu: “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Yesu analirudia jibu lake kuonesha kwamba Petro amejibu vizuri. Hata hivyo, yaonekana Petro hakujua sawasawa maana ya jibu alilotoa. Ni dhahiri Petro amemwona Yesu kuwa ni pekee kupita wengine wote, ni mwana wa Daudi, ni mpakwa wa Mungu, ni Masiha, lakini anafikiri kutokana na vigezo vya ulimwengu huu. Hajaelewa kuwajibika anakodaiwa awe nako mbele ya huyo Yesu. Yesu anamweleza: “Heri wewe Simoni Bar-Yona, kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.”

Maana yake, alichojibu Petro hakitokani na kufikiri kwake, bali kwa ufunulio unaopatikana kwa walio na moyo safi. Hao ndio pekee wanaoweza kuelewa na kupokea ukweli unaotoka kwa Mungu. “Heri wenye moyo safi kwani watamwona Mungu.” Swali hili la pili yabidi kujiuliza hata sisi katika uchaguzi wa maisha yetu. Haitoshi tu kumkiri Yesu ni nani, bali hasahasa kujihoji Yesu anachukua nafasi gani katika maisha yangu binafsi, katika kazi na shughuli zangu, ninapotembea, ninaposoma, ninapolala, katika familia yangu, katika burudani zangu nk.

Baada ya kujihoji hivyo sasa ona jibu la Yesu kwa Petro: “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu,” (Mt 16:18-19). “Petrus” maana yake ni jiwe au tofali; lakini Petra maana yake ni mwamba. Yesu anamwita Petro kuwa ni Petrus. Katika Agano jipya Jiwe au Mwamba huo ni Yesu Kristo peke yake. Juu ya mwamba huo Mungu amejenga kanisa lake: “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.” (Waef. 2:20).

Aidha, “Wote wakanywa kinywaji kilekile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.” (IKor. 10:4). Yesu anaongea juu ya ungamo la imani ya Petro mtume, na ungamo hilo ndilo linalomfanya mtume huyu awe jiwe hai la kujenga kanisa lenye msingi wake juu ya mwamba. Humo hekaluni mtatolewa sadaka inayompendeza Mungu.

Yesu anataka kusema: “Wewe umekuwa wa kwanza kuungama imani juu ya yangu, wewe ni tofauli hai la kwanza katika ujenzi wa kanisa hai ambalo jiwe lake la msingi ni Mimi mwenyewe.” Imani aliyoungama Petro inamfanya awe jiwe hai la kwanza lakini siyo la mwisho katika kujenga imani hii mpya. Kwa hiyo kila mkristu anayeungama imani ya Petro juu ya Kristu aliye Bwana wa uzima, huyo naye ni jiwe au tofali.

Kisha Yesu anaendelea kusema: “wala milango (nguvu za) ya kuzimu haitalishinda” (Mt 16:19). Injili inataja neno kuzimu (Khades) lenye kumaanisha jehena au pango chini ya ardhi wanakoishia wema na wabaya. Kwa hiyo kuzimu au Khades ni kifo au utawala wa kifo. Ni kifo kinachoshindana na maisha au uzima ule wa Kristu na kifo hicho hakitautawala uzima wa Kristu. Kisha Yesu anasema: “Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni”.

Ufalme wa mbingu ni ulimwengu mpya uliopokea ujumbe mpya wa Kristu. Petro alipewa funguo ambazo kwa kiyahudi humaanisha “kuacha wazi au kufungua”. Kwa hiyo Petro na imani yake juu ya kristu yamaanisha kuhubiri, kuwafungua watu mioyo na akili yao kusikia na kumpokea Kristu.

Tungeweza pia kusema kwamba utume wa kufunga na kufungua tumepewa sisi wakristu wote. Yaani kutangaza ujumbe wa Mungu ambao Kristu ameuleta duniani. Petro aliungama imani na akawa mtunzaji wa ukweli huu wa Bwana. Paulo pia alikuwa naye katika kuitangaza imani hiyo. Kumhubiri na kumshuhudia Kristu katika maisha yetu.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.