2014-06-28 15:32:19

Ni hija ya kiekumene ya maisha ya kiroho inayosimikwa katika damu ya mashahidi


Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru kwa namna ya pekee Patriaki Bartholomeo wa kwanza pamoja na Sinodi ya Costantinopoli kwa kutuma ujumbe maalum kwa ajili ya maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani. Baba Mtakatifu ameyasema hayo, Jumamosi asubuhi, alipokutana na kuzungumza na Ujumbe wa kiekumene kutoka katika Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli.

Anasema bado anaendelea kuhifadhi moyoni mwake kumbu kumbu ya matukio ambayo yaliwakutanisha na Kaka yake Bartholomeo wa kwanza wakati wa hija yake ya kitume Nchi Takatifu, mahali alikozaliwa Yesu, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Patriaki Anathegoras na Papa Paulo VI walipokutana na kusali, mwanzo wa hija ya majadiliano ya kiekumene inayoendelea hadi leo hii ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbuka kwa umakini mkubwa walipokutana na kusali kwenye Kaburi Takatifu, kwa kugusa msingi wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, hija ambayo ilihitimishwa kwenye kaburi la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa kusali ili kuombea amani na upatanisho huko Mashariki ya Kati, tukio ambalo liliwashirikisha Marais wa Israeli na Palestina. Matukio yote haya ni neema ya Mungu, iliyowawezesha kukutana na kusali, ili kuonjesha upendo wa Kristo unaowaunganisha pamoja pamoja na kuendelea kuonesha utashi wa kutaka kusonga mbele katika hija ya majadiliano ya kiekumene ili kuweza kufikia umoja kamili.

Baba Mtakatifu anasema, umoja miongoni mwa Wakristo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu pamoja na nguvu na neema ya Roho Mtakatifu inayowawezesha kuangaliana kwa macho ya kiimani, ili kujitambua mintarafu mpango wa Mungu wa milele yote na wala si kwa yale yaliyojitokeza katika historia ya maisha ya Kanisa na dhambi zilizowapelekea hadi wakafika hapo walipofikia.

Ikiwa kama Wakristo watajifunza kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu ili awaongoze, daima wataendelea kuangalia katika "miwani" ya Mwenyezi Mungu, kwa kutembea, kushirikiana na kutenda kwa umoja katika medani mbali mbali za mambo yanayowaunganisha hadi wakati huu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, mtazamo huu wa kitaalimungu unarutubishwa na imani, matumaini na mapendo; una uwezo wa kutoa tafakari ya kina kuhusu elimu ya Mungu "Scentia Dei", kwa kushiriki mtazamo wa Mungu alionao juu yao. Ni tafakari inayoweza kuwasaidia kukaribiana zaidi katika umoja hata kama wanatoka katika mielekeo tofauti.

Baba Mtakatifu anasema anaendelea kusali kwa ajili ya mafanikio ya Tume mchanganyiko ya kimataifa katika mchakato wa majadiliano ili kuendelea kufanya tafakari hii kwa kupiga magoti. Ni Tume inayoangalia umuhimu wa Sinodi, Umoja wa Kanisa la Kiulimwengu na Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro; tema ambazo hazipaswi kubakia zinakumbatiwa katika masuala ya wasomi na kinzani, bali Wakristo wanapaswa kuonesha ujasiri na imani kwa kazi ya Roho Mtakatifu, kwa kumpatia nafasi ya kuliangalia Kanisa ambalo ni mchumba wa Kristo, anayetembea katika hija ya kiroho ya kiekumene, inayoimarishwa kwa njia ya mashahidi walioyamimina maisha yao kwa kumuungana Kristo na hivyo, kujenga majadiliano ya kiekumene kwa njia ya damu yao.

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wajumbe wa Kiekumene kutoka Costantinopoli, kwa heshima, urafiki na upendo anapenda kwa mara nyingine tena kuwashukuru na kuwataka kumfikishia salam na matashi mema, Patriaki Bartolomeo wa kwanza. Anawaalika kumwombea katika maisha na utume wake. Baadaye kidogo, wajumbe hawa pamoja na Baba Mtakatifu Francisko wamebadilishana zawadi.All the contents on this site are copyrighted ©.