Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican, Ijumaa tarehe 27 Juni 2014 ameongoza ujumbe wa Vatican
katika kutia sahihi Itifaki ya makubaliano kati ya Vatican na Serikali ya Serbia kuhusu
Serikali kushirikiana na Kanisa katika utoaji wa elimu ya Sekondari. Ujumbe kutoka
Serikali ya Serbia uliongozwa na Bwana Veljko Odalovic, Katibu mkuu wa Wizara ya Mambo
ya nchi za nje.
Itifaki hii inawahamasisha viongozi wa pande hizi mbili kushirikiana
kwa karibu zaidi ili kuendeleza elimu ya sekondari kwa njia ya mawasiliano ya mara
kwa mara. Itifaki hii inatambua pia vyeti vinavyotolewa kwa wanafunzi wanaosoma katika
shule za Sekondari zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa nchini Serbia. Itifaki ya
Mkataba huu itaanza kutekelezwa baada ya pande zote mbili kuhitimisha masharti, utekelezaji
wake na masuala ya fedha. Itifaki inalipatia Kanisa uwezo wa kuanzisha na kuendeleza
shule za Sekondari zinazofundisha masomo ya Kanisa na elimu dunia.
Mwishoni,
taarifa kutoka Belgrade inasema kwamba, Itifaki hii itaanza kutumika rasmi mara tu
baada ya pande hizi mbili kukamilisha masharti yote yaliyotajwa katika itifaki ya
ushirikiano kati ya Serikali ya Serbia na Kanisa Katoliki nchini Serbia.