Afrika iwe na msimamo mmoja katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi!
Nchi za Afrika zinatakiwa kuwa na msimamo mmoja kuhusu jinsi ya kukabiliana na madhara
ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa barani Afrika. Misimamo huo wa Afrika unatarajiwa kuwasilishwa
kwenye mkutano mkubwa wa Dunia kuhusu masuala ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa unaotarajiwa
kufanyika New York, Marekani Mwezi Septemba, 2014.
Akiwakilisha ripoti ya
Kamati ya Viongozi wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani, tarehe 27
Juni,2014 katika Mkutano wa Viongozi wa Afrika (AU), Rais Kikwete amesema kamati yake
inataka kujikita na kujihusisha na masuala yanayohusu fedha na teknolojia, hatua za
kupunguza madhara, na hatua mtambuka ambazo zitahusisha progamu za vijana, wanawake
na hata kuhusisha Balozi mbalimbali za Afrika katika suala zima la mabadiliko ya hali
ya hewa na pia kuhusisha Jumuiya ya Kimataifa na kufuatilia mapendekezo mbalimbali.
Rais ameziasa Nchi za Afrika kuwa na utashi wa kisiasa na lengo la pamoja
katika kukabiliana na suala hili ili kufanikisha lengo la dunia la hali ya hewa katika
kipindi cha nusu ya pili ya karne ijayo. Rais amesema, ili kufanikisha juhudi mbalimbali,
Bara la Afrika linahitaji msaada mkubwa wa fedha na teknolojia ya kisasa.
Mapema
katika kikao cha Kamati ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa ambacho pia kimehudhuriwa na
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bwawa Ban Ki Moon, Rais Kikwete amesema mkutano
ujao wa UN kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani ni chachu ya makubaliano ya Mkataba
wa Hali ya Hewa ifikapo 2015. Ripoti za karibuni kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa
inaonesha kuwa hali ya Kilimo, Afya, Maji na Nishati ziko hatarini na kwamba joto
duniani limepanda kwa sentigredi 0.85, hali ambayo inaashiria hali mbaya. Mkutano
wa Viongozi wa Afrika (AU) umekamilika tarehe 27 Juni 2014 majira ya jioni.