Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya
Mashariki, Alhamisi jioni tarehe 26 Juni 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki
cha Bethlehemu. Ibada hii imewashirikisha wajumbe wa bodi ya wadhamani na baadhi ya
wanafunzi, ambao pia walipata bahati ya kuhudhuria Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko,
siku ya Jumatano.
Kardinali Sandri katika mahubiri yake amekazia kuhusu umuhimu
wa Fumbo la Msalaba, linaloonesha jinsi ambavyo Yesu mwenyewe alijisadaka na kuwakirimia
wanafunzi wake chakula cha uzima wa milele na Roho Mtakatifu, anayewawezesha kuwamegea
wengine upendo kama unavyojionesha katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Bethelehemu.
Huu ni ushuhuda wa imani tendaji, unaojionesha kwa majitoleo ya watu mbali
mbali ili kuhakikisha kwamba, vijana wanapata elimu itakayowawezesha kuwa na utimilifu
wa maisha. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuendelea kuwa waaminifu kwa Mungu na kwa
binadamu, kwa kuendeleza juhudi za kuwapatia vijana elimu, kwa utukufu wa Mungu unajionesha
kwa mwanadamu aliye hai.
Kardinali Sandri anasema kwa njia ya upendo kwa Kristo
na vijana wa dini mbali mbali wanaosoma Chuo hapo, Kanisa linatekeleza dhamana ya
kuwajengea vijana matumaini na kwamba, vijana nao wahakikishe kuwa hakuna mtu anayewapora
matumaini haya kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Chuo kikuu kiwe ni mahali
pa ujenzi wa misingi ya haki, amani, umoja na upatanisho wa kitaifa. Vijana wanaofundwa
chuoni hapo wahakikishe kwamba, wanabomoa kuta za utengano kati ya watu na badala
yake upendo na amani vitawale mioyo ya watu!