2014-06-27 09:59:51

Utakatifu wa Mapadre!


Askofu mkuu Celso Morga Iruzubieta, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika maadhimisho ya Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu sanjari na Siku ya Kimataifa kwa ajili ya kuombea utakatifu wa Mapadre anasema kwamba, kuna haja kwa Mapadre kuhakikisha kwamba, wanajitosa kimasomaso kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kwa kuwahudumi kikamilifu wale ambao Mama Kanisa amewawekea mbele yao.

Mapadre ni kati ya mihimili mikuu ya utangazaji wa Injili ya Furaha kazi ambayo hawana budi kuipatia kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wao anasema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Injili ya Furaha. Daraja Takatifu ni huduma ya upendo inayofumbatwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu ambalo Yesu amelikabidhi Kanisa ili liendelee kuliadhimisha kwa ajili ya ukumbusho wake.

Mapadre wanaweza kutekeleza utume huu kutokana na neema waliyokirimiwa na wala si utakatifu au mastahili waliyo nayo kama binadamu! Ikumbukwe kwamba, hata waamini walei kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki ukuhani, ufalme na unabii wa Kristo, kumbe ni jukumu la Mapadre kuishi Upadre wao kwa moyo wa unyenyekevu na shukrani kwa Kristo na Kanisa lake.

Mapadre wamepewa dhamana na utume wa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa ajili ya sifa na utukufu kwa Mungu na utakatifu kwa binadamu. Hapa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka ndiye anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si Padre anayeadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Mapadre waendelee kujifunza kutoka kwa Yesu Kristo mchungaji mwema, mpole na mnyenyekevu wa moyo, aliyekuja si kwa ajili ya kuhudumiwa bali kuhudumia na kutoa uhai wake ili uwe ni fidia kwa wengi.

Mapadre waoneshe upendo na ukarimu wa kichungaji; wawaonjeshe waamini wao ile furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, wawakumbatie na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; wawafariji na kuwasaidia wote, ili kweli Padre aweze kuwa ni mtu wa Mungu, mshauri wa amani, rafiki wa waamini na mtu mwenye hekima na busara, ambaye watu wanaweza kumtumaini katika furaha na magumu ya maisha yao!

Kishawishi kikubwa kwa Mapadre wa nyakati hizi ni kutaka kukimbia majukumu na utume wao wa Kipadre, ili kutafuta usalama na uhakika wa maisha na kusahau kwamba, wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa mataifa. Kuna kishawishi cha Mapadre kutaka kuficha utambulisho wao kwa kutafuta uhuru usiokuwa na mipaka, uhuru ambao wakati mwingine unaweza kuwatumbukiza katika majanga ya maisha.

Mapadre watambue kwamba, wao ni sauti ya kinabii, ni watu walioteuliwa miongoni mwa watu kwa ajili ya mambo ya Mungu ni watu wanaotenda kwa ajili na pamoja na Jumuiya ya waamini na kamwe si watu wanaotekeleza majukumu yao pweke pweke!

Padre ajitahidi kuwashirikisha makleri na waamini walei upendo na utume wake. Mapadre na waamini wapambane kufa na kupona na vishawishi vya ubinafsi na upweke katika utekelezaji mikakati ya shughuli za kichungaji. Kanisa linatumwa kutangaza Injili ya Furaha kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji!








All the contents on this site are copyrighted ©.