2014-06-27 08:14:16

Usiwasahau maskini!


Jumapili tarehe 29 Juni 2014 Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Sherehe za Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hawa ni “vigogo” wa imani waliojitosa kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa mataifa kwa njia ya mahubiri, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, wakawa tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Hii ni Jumapili ambayo Baba Mtakatifu anatarajiwa kutoa Pallio Takatifu kwa Maaskofu wakuu wa Majimbo makuu walioteuliwa hivi karibuni, kama kielelezo cha umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii pia ni siku ya mshikamano kwa kuonesha upendo kwa Baba Mtakatifu kwa njia ya sala, lakini kwa kuchangia katika Mfuko maalum wa huduma ya mshikamano na upendo unaotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, sehemu mbali mbali za dunia.

Mchango huu unaotolewa na waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema unamwezesha Baba Mtakatifu kuwasaidia watu waliokumbwa na majanga asilia kama vile matetemeko ya ardhi, mafuriko, njaa, ukame. Ni msaada unalenga kumsaidia mtu mzima katika mahataji yake: kiroho na kimwili, kwa kuchangia maboresho katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa kuwajengea uwezo ili kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri mkuu.

“Usiwasahau maskini” ni maneno ambayo Kardinali Claudio Hummes alimwambia Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Maneno haya yakaingia na kunata katika akili na moyo wa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye leo hii maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni anawapatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake, si kwa maneno tu bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Papa akamchagua Mtakatifu Francisko wa Assis mpenda amani, mazingira na mhudumu wa maskini kuwa msimamizi wake, leo hii mjini Vatican wimbo umebadilika, mwenye macho aambiwi tazama!

Siku ya Upendo wa Papa ilianzishwa kunako tarehe 8 Agosti 1871 na Papa Pio IX katika Waraka wake wa kichungaji “Saepe Venerabilis” na tangu wakati huo, kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Kanisa linashikamana na Papa kuonesha upendo na ukarimu kwa kuchangia mfuko unaogharimia shughuli mbali mbali za upendo zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu sehemu mbali mbali za dunia.

Nawe unaweza kushikamana na Papa kwa kuchangia katika mfuko huu! Kwa njia hii, unashiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya kwani maisha na utume wa Kanisa unaendelea kupanuka siku hadi siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.