Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu sanjari na siku ya kuombea
utakatifu wa Mapadre iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2002.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akatangaza na kuadhimisha Mwaka wa Mapadre kati
ya Mwaka 2010-2011.
Bado kuna
changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba, Mapadre wanakuza na kudumisha uaminifu wao
kwa Kristo na Kanisa lake kwani Mapadre ni Watu wa Mungu kwa ajili ya Watu. Padre
ni mhudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, ni mlezi wa Taifa la Mungu. Kanisa
linawaalika waamini kuwaombea Mapadre kwani linatambua kwamba, zawadi hii kubwa imehifadhiwa
kwenye vyombo vya udongo.
Askofu Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar
anasema, Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, sanjari na Siku ya kuombea Utakatifu
wa Mapadre, Zanzibar kama Kanisa mahalia linapenda kusisitizia umuhimu kwa Mapadre
kuwa wavumilivu, kuendelea kuwa Mashuhuda thabiti wa imani kwani Mapadre wakiyumba
katika imani, amani inayotangazwa inaweza kutoweka pia. Mwaliko ni kwa Mapadre kuishi
wito wao kwa kuendelea kuwa kweli ni mashuhuda katika medani mbali mbali za maisha!
Askofu
Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mawosia
yake ya kichungaji, anawataka Makleri kumwiga Yesu Kristo aliyejipambanua kwa kuwa
ni kiongozi na mchungaji mwema; mwaminifu, mtiifu na mwenye huruma na mapendo pasi
na mipaka. Hii ni changamoto na mwaliko kwa Mapadre kuhakikisha kwamba, wanamwiga
na kumfuata Kristo katika uaminifu, upendo, unyofu, unyenyekevu, huruma na mapendo.
Mapadre
wawe na mvuto na mashiko ili watu waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu. Mapadre
wawe ni mfano katika maneno na matendo yao kwa kumfuasa Kristo ambaye ni mfano bora
wa utakatifu wa maisha, Bwana, Mwalimu na Mlezi wa Mapadre.