2014-06-27 06:51:35

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 13 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa kipindi tafakari masomo Dominika, niko pamoja nawe tena katika Dominika hii ya XIII ya mwaka A, kukushirikisha furaha yangu toka meza ya Neno la Mungu. Mwaliko toka Neno lenyewe ni kwamba mkristu aalikwa kuwa na upendo mkuu kwa Mungu kuliko vitu vingine vyote. RealAudioMP3


Ni katika kumpenda Mungu mkristu aweza kutoa huduma kwa wengine na kwa njia hiyo kuendelea kumpokea Mungu zaidi na zaidi. Basi katika kutenda hayo Mungu anatangaza uhakika wa thawabu kwa mwenye kutenda hilo.


Katika somo la kwanza toka kitabu cha Pili cha Wafalme tunakutana na Nabii Elisha katika nchi ya Shunemu, pamoja na mwanamke mmoja aliyekuwa mgumba lakini mwenye ukarimu na cheo! Mji wa Shunemu ulikuwa umejengwa kando ya mlima na wakazi wake walikuwa wakulima ambao kwa njia ya kilimo walisadikika kujikusanyia utajiri. Mara kadhaa Nabii Elisha alikuwa akipita mbele ya nyumba ya familia moja ambayo haikuwa na mtoto. Kwa mazoea ya kupita pale mara kadhaa mama anaingiwa furaha na kuitwa na ukarimu wa kimama na anamkaribisha chakulani Elisha.


Si hilo tu bali mama huyu anamwomba mmewe ambaye alikuwa mzee wamtayarishie chumba mtumishi wa Mungu huyu ili kila apitapo apate mahali pa kulala. Toka tendo hili la ukarimu Mungu atamjalia mama huyu mtoto na hivi si tena mkiwa wala mgumba bali ukarimu umezaa! Mama huyu anapomkaribisha Nabii Elisha anatangaza kwetu sisi namna ya ushiriki wake katika mpango na kazi ya Mungu. Kwa ushiriki huu basi Mungu lazima atatoa zawadi nzuri na hivi kujisikia mama mkamilifu.


Mpendwa msikilizaji tunapata kujifunza kuwa, katika kuhudumia kuna baraka na heri za Mungu. Si hilo tu bali pia Elisha anatupa picha ya kimisionari, yaani kuacha nchi yako na baadaye kukutana na familia nyingine kubwa zaidi ndiyo Kanisa la Mungu. Kumbe hakuna haja ya kuogopa kunakotokana na kuacha familia zetu kwa maana ni lazima Mungu atatoa tu kwa watenda kazi wake.


Katika somo la Pili Mtakatifu Paulo anawaandikia Warumi akiwakumbusha maana ya ubatizo, yaani ni kufa katika mauti ya Kristu na kufufuka naye. Baada ya ufufuko kama Bwana alivyo mtakatifu, nasi tunaalikwa kuenenda katika upya wa maisha, yaani ule upya tulioupata kwa njia ya Neema ya Utakaso. Ni katika mantiki hiyo ya ufufuko nasi tutaishi milele pamoja na Kristu. Tunakuwa wapya kwa maana kwa njia ya ubatizo tunazika mambo ya kale na kuanza maisha mapya.


Mpendwa msikilizaji, jambo la upya katika litrujia ya ubatizo kwa sasa halionekani vizuri kama zamani ambapo mmoja alizamishwa katika mto na hivi alipoibuka ilisadikika kwamba dhambi na mizigo ya zamani imechukuliwa na mkondo wa maji. Kwa ubatizo maana yake tunakwenda pamoja na Kristu kaburini na wakati anapofufuka tunatoka pamoja naye tukiwa wapya! Basi kama ambavyo Kristu harudi tena katika mauti na mkristu vivyo hivyo hapaswi kurudi katika ukale wa maisha bali anazaliwa upya na kuishi maisha mapya.


Katika Injili ya Matayo, Bwana anafundisha namna mbatizwa ambaye amekufa katika mauti ya Bwana na kufufuka naye anavyopaswa kuishi upendo. Upendo wake unapaswa kuwa wa kweli na sio wa kibaguzi, yaani upendo uliojaa huduma kwa wengine. Namna ya kuishi mapendo haya ni kujitahidi kujibandua katika mgandamizo wa tamaduni na hivi kuanza na Mungu kila siku safari ya upendo. Mpendwa, Upendo ambao Bwana anautaka ni ule ambao unahudumu waliowahitaji na walio katika huduma ya Neno la Mungu.


Mpendwa msikilizaji, Bwana akitaka kukamilsha hili, katika sehemu ya kwanza ya Injili anasema, ni lazima anayetaka kunifuata na kuuishi upendo ajibandue katika tamaduni na mizigo ya ndugu na mambo kama hayo na kuwa huru tayari kwa misioni. Katika hili yawezekana kuona mbegu ya kukataa amri ya 4 ya Mungu! Bwana hayuko katika mantiki hiyo yeye anachotafuta ni kwamba mfuasi lazima awe thabiti katika ufuasi wake na si kubabaisha au kuwa nusunusu!


Katika sehemu II ya Injili, Bwana anakazia suala la huduma kwa watenda kazi katika shamba lake. Anasema atendaye mema kwa hawa watumishi anitumikia mimi. Hapa tunapata muunganiko pamoja na somo la kwanza pale tunapomwona Elisha nabii akihudumiwa na familia moja huko alikokuwa akifanya utume wake. Hata hivyo yafaa kuelewa vema jambo hili, yakwamba hoja kuu ni kushiriki katika utume wa Mkombozi wa ulimwengu yaani Bwana wa mavuno mwenyewe.


Ninakualika kushiriki kazi ya Bwana, maana ni kwa njia hiyo nawe unatayarisha neema na baraka tele kama alizozipata mama mgumba aliyemhudumia Nabii Elisha katika somo la kwanza. Ninakualika tena kuwa mtu ambaye unaweza kusifu na kukuza utukufu wa Mungu kwa njia ya mapadre, masisita wanaohudumia taifa la Mungu popote duniani.

Kumbuka kuwaombea hasa wale wanaofanya kazi katika nchi ambapo uhuru wa kuabudu umebanwa kwa asilimia zote na hasa kwa kile kinachoitwa madhulumu ya kidini. Kwa kuwaombea utakuwa unashiriki kikombe kimoja tukibarikisho kama ushirika wa Kristu na hivi kuwasaidia kujaliwa na mastahili ya msalaba wa Bwana.


Nikutakie furaha na heri na hasa ukakue katika moyo wa huduma kwa Kanisa na kwa familia yako na kisha mwisho wa maisha yako hapa duniani upate uzima wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.