Sayansi inaweza kuchangia kudumisha misingi ya haki na amani!
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, sayansi inaweza kuwa ni chombo muhimu
sana katika kukuza na kuendeleza misingi ya haki na amani duniani, kumbe, ni vyema
na haki ikiwa kama watu wengi zaidi wataweza kufaidika na tafiti pamoja na majiundo
makini ya kisayansi yanayotolewa duniani. Hii ni changamoto kubwa inayowahusisha wadau
mbali mbali, lakini kwa namna ya pekee, wanasayansi na watalaam.
Ni changamoto
iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 26 Juni 2014 alipokutana
na kuzungumza na wanafunzi 25 kutoka katika Kituo cha Unajimu cha Vatican, kilichoko
mjini Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma. Kituo hiki kilianzishwa kunako mwaka
1986, ili kutoa fursa kwa wanafunzi waliokuwa wanahitimu masomo yao kutoka kwenye
Vyuo vikuu kunoa ubongo, kujenga na kudumisha urafiki na majaalimu pamoja na wanafunzi
kutoka katika nchi ishirini na tatu. Ni fursa ya kujifunza kazi ya uumbaji na kwamba,
wanayo kila sababu ya kuwashukuru wafadhili waliowawezesha kutimiza ndoto yao!
Baba
Mtakatifu anasema, Kituo cha Unajimu cha Vatican ni mahali ambapo vijana kutoka sehemu
mbali mbali za dunia wanajadiliana, wanashirikiana na kusaidiana kutafuta ukweli kuhusu
nyota. Kanisa kwa upande wake pia linaendelea kufanya majadiliano na wanasayansi ili
kuchangia katika tafiti mbali mbali kwa mwanga wa imani, kwa kutambua zawadi kubwa
ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu na kwamba, anafurahia kuwaona watoto wake
wakikua katika umri na hekima.