Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba, amri kuu ndiyo hii: Mpendane, kama nilivyowapenda
ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili
ya rafiki zake.
Naam, “Upendo
mkuu” ndiyo kauli mbiu itakayoongoza Onesho la Sanda Takatifu, Jimbo kuu la Torino,
Kaskazini mwa Italia. Onesho hili litafanyika kuanzia tarehe 19 Aprili na tarehe
24 Juni 2015, siku ambazo waamini na watu wenye mapenzi mema wanaweza kupata nafasi
ya kusimama kidogo na kufanya tafakari ya kina kuhusu Sanda Takatifu.
Sanda
hii inayomwonesha mtu aliyeteseka; akapigwa mijeledi na kuvishwa taji la miba. Ni
mtu aliyefariki dunia, lakini baada ya siku tatu, akafufuka kutoka katika wafu. Upendo
ndiyo changamoto endelevu inayotolewa na Krisdto pamoja na Kanisa lake kwa watu wa
nyakati zote. Kila mtu anaalikwa kujisadaka kwa ajili ya jirani zake. Hivi ndivyo
anavyosema Askofu mkuu Cesare Nosiglia, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Torino.
Changamoto
ya mtu kujisadaka kwa ajili ya wengine ni endelevu na inamgusa kila mtu kadiri y anafasi
na dhamana yake ndani ya Kanisa na Jamii inayomzunguka. Watu wanaweza kujisadaka kwa
kutoa muda wao kwa ajili ya matendo ya huruma kwa Mungu na jirani: kwa kuwatembelea
na kuwahudumia wagonjwa na wazee wasiojiweza. Sanda Takatifu iwakumbushe waamini na
watu wenye mapenzi mema taabu na mateso ya wagonjwa wanaokufa hospotalini kwa kukosa
huduma makini, woga na upweke.
Waamini waguswe na mateso ya wagonjwa, ili
waweze kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa
sura na mfano wa Mungu. Sanda Takatifu iwachangamotishe watu kutoa huduma makini kwa
wale wanaowahudumia: kiroho na kimwili; waoneshe moyo na mshikamano wa udugu na upendo,
kwa kutembea katika shida na mahangaiko ya wagonjwa hawa. Sanda Takatifu inagusa undani
wa maisha ya mtu, ambaye baada ya kuiona kamwe hawezi kubaki kama alivyokuwa bila
ya kuguswa na mahangaiko ya watu.
Askofu mkuu Cesare Nosiglia anasema kwamba,
Sanda Takatifu ya Torino ina uhusiano mkubwa na mateso na kifo cha Yesu, mwaliko wa
kuthamini na kuenzi maisha ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watu
wasikubali kukumbatia utamaduni wa kifo, bali wasimame kidete kulinda na kutetea zawadi
ya uhai kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Watu waguswe na mateso ya wagonjwa wanaoishi
kwa matumaini; watu ambao daima wanakiona kifo usoni pao!
Pengine wagonjwa
kama hawa si watu wa kulalama; ni watu ambao wamepokea na kuukubali mpango wa Mungu
katika maisha yao! Waamini wanapotembelea Wodi za wagonjwa mahututi, waguswe ili kuwaonjesha
upendo, kama walivyofanya watakatifu kama Mama Theresa wa Calcutta, Mtakatifu Vincent
wa Paulo na watu wengine wengi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya watoto yatima
na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi; wale wanaosimama usiku na mchana wakisikiliza
kilio cha damu kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu; watu ambao wanataka
kuenzi Injili ya Uhai. Sanda Takatifu ichochee moyo wa toba na wongofu wa ndani; moyo
wa huruma na mapendo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.