Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema
kwamba, vitendo vya kigaidi vinavyoendeshwa na Kikundi cha Boko Haram vina madhara
makubwa kwa maisha ya watu na mali zao.
Ni matumaini
ya Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kwamba, wasichana waliotekwa nyara wataweza
kuachiliwa huru mara moja na kwamba, kuna haja kwa Serikali ya Nigeria kusimama kidete
kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu, haki, amani na usalama wa wananchi wake.
Askofu
mkuu Kaigama ameyasema hayo hivi karibuni katika Kongamano la Kimataifa lililoandaliwa
na Shirika la Kipapa linalosaidia Makanisa hitaji kuhusu uhuru wa kidini, huko nchini
Malta. Hivi karibuni, wasichana wa shule 276 walitekwa nyara na kikundi cha Boko
Haram, kati yao 53 ndio waliofanikiwa kuwatoroka watesi wao. Wasichana hawa ni waamini
wa dini mbali mbali nchini Nigeria, kumbe, lengo si kwa ajili ya kuwasilimisha Wakristo
tu, bali kuhakikisha kwamba, Nigeria inatawaliwa na “Sharia” za dini ya Kiislam.
Boko
Haram inataka kusambaratisha tunu msingi za maisha ya Kikristo nchini Nigeria kwa
madai kwamba, zinataka kurithisha utamaduni kutoka nchi za Magharibi ambazo kadiri
ya Boko Haram ni tamaduni harem. Hili ni jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa na
haki msingi za binadamu pamoja na uhuru wa kuabudu. Watu wanapaswa kuheshimiana na
kuthaminiana hata katika tofauti zao kwani tofauti hizi si kwa bahati mbaya bali ni
mpango wa Mungu, ili watu waweze kutajirishana.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Nigeria linabaianisha kwamba, tangu mwaka 2009 Boko Haram ilipoanza kufanya mashambulizi
ya kigaidi nchini Nigeria, watu wengi wamepoteza maisha na mali pamoja na kusababisha
uharibifu mkubwa wa miundo mbinu. Vitendo vya kigaidi vinavyoendeshwa na Boko Haram
vimewafanya wananchi wengi wa Nigeria kukosa imani na Serikali, kwani imeonesha udhaifu
mkubwa katika kudhibiti vitendo vya kigaidi nchini humo.
Jambo hili linaonesha
kwamba, pengine kuna baadhi ya viongozi wa Serikali na wanasiasa wanatetea masilahi
binafsi, lakini wakumbuke kwamba, watu wanaendelea kupoteza maisha na mali zao. Rasilimali
fedha na watu iliyotengwa kupambana na Boko Haram imetumika vibra kutokana na kukithiri
kwa tabia ya rushwa na ufisadi nchini Nigeria.
Jumuiya ya Kimataifa haina
budi kuisaidia Nigeria kupambana na Boko Haram kwa kufanya upembuzi yakinifu wa mahali
ambapo Boko Haram wanapata silaha za moto ambazo zimekuwa ni tishio kwa usalama na
maisha ya wananchi wa Nigeria. Ni haki na vyema kuwafahamu watu wanaofadhili vitendo
vya kigaidi nchini Nigeria ili waweze kushughulikiwa kikamilifu na Jumuiya ya Kimataifa,
kwani ni jambo la kusikitisha kuona kwamba, kuna watu wanaotaka kupata utajiri wa
haraka haraka kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia.
Kumbe, operesheni
ya kijeshi iliyoanzishwa na Serikali bado haijafua dafu kwa Boko Haram. Ni vyema ikiwa
kama Serikali itaibua mbinu mkakati wa kupambana na umaskini, ukosefu wa fursa za
ajira pamoja na rushwa kwani haya ni mambo ambayo yanaendelea kuchochea vitendo vya
kigaidi vinavyofanywa na Boko Haram.