2014-06-27 15:39:13

Kamati ya Misitu yamaliza mkutano wake mjini Roma


Mkutano wa ishirini na mbili (22) wa Kamati ya Misitu (Committee on Forestry-COFO) ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) umefanyika mjini Roma, Italia kwenye makao makuu ya Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO. Hii ni kawaida kwa mikutano ya nchi wanachama wa FAO kufanyikia mjini Roma, Italia kwani hapa ndipo yalipo Makao makuu ya FAO.

Kamati ya Misitu (COFO) inawezekana ikaeleweka kwa wengi kama ni kamati ndogo ukweli ni kwamba tunaposema Kamati ya misitu duniani tunamaanisha ni nchi wanachama wa FAO ambazo hukutana na kwa pamoja kuweza kuzungumza na kushauriana juu ya masuala mbalimbali yanayohusu sekta za misitu, wanyamapori na kwa upande fulani nyanda za malisho ya mifugo hasa kwa maeneo kame.

Kwa mara ya kwanza kikao cha Kamati ya Misitu duniani kilifanyika mwaka 1977. Kikao cha 22 COFO kimefanyika Rome, Italia tarehe 24 hadi 27 Juni 2014 na kuhudhuriwa na nchi wanachama 125 na mashirika ya kimataifa yapatayo 10 yameshiriki na kuweza kutoa michango yao pale wawakilishi wa mashirika hayo walipoona ni muhimu kufana hivyo.

Mkutano wa Kamati uliambatana na shughuli mbalimbali za Juma la Misitu Duniani (World Forest Week) ikiwemo na mijadala tofauti na ile ya Mkutano wa COFO hasa iliyoongozwa na mashirika ya kimataifa yanayojishughulisha na masuala mbalimbali ya misitu pamoja na wanyamapori ikiwepo utafiti, mafunzo, masuala ya kijamii na uhifadhi wa mazingira.


Mkutano ulifunguliwa rasimi tarehe 23 Juni 2014, kuanzia saa nne asubuhi kwanza, kwa Mwenyekiti wa Mkutano wa Kamati wa 21: Dkt. Felician Kilahama kutoka Tanzania alipotimiza wajibu wake kwa kuwakaribisha rasimi kwenye mkutano wajumbe wote wa mkutano wakiwemo Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wageni Mashuhuri na wawakilishi wa nchi na wale wa mashirika ya kimataifa. Pili, Mwenyekiti wa COFO 21 Dr. Kilahama aliweza kutamka rasmi kuwa sasa Mkutano wa nne wa Juma la Misitu Duniani (World Forest Week) na Mkutano wa 22 wa Kamati ya Misitu (COFO) sasa vimefunguliwa rasmi.

Baada ya hapo mwenyekiti wa COFO-21 Dkt. Kilahama, aliendesha shughuli za ufunguzi kwa kuwakaribisha wageni waalikwa sita kutoka sehemu mbalimbali duniani ili waweze kutoa nasaha zao. Awali ya yote Dkt. Kilahama alimkaribisha Mhe. Jose Graziano da Silva, Mkurugenzi Mkuu, FAO aweze kusema machache na kuweza kuzinduliwa rasimi Balozi Mteule wa FAO kwa masuala ya Mazingira na misitu mwana wa Mfalme: H.R.H Prince Laurent kutoka Ubelgiji.
Katika hotuba yake H.R.H Prince Laurent aliishukuru FAO kwa kumpa heshima hiyo ya kuwa Balozi mteule katika Mazingira na misitu na akaahidi kuwa atatoa mchango wake ipasavyo. Mwenyekiti wa COFO-21 Dr. Felician Kilahama, pia alimpongeza Mhe. Prince Laurent wa Belgium kwa kazi hiyo kwa faida ya dunia nzima. Vilevile, Dr. Kilahama alimwomba atakapoonza kufanya kazi atoe kipaumbele kwa Bara la Afrika maana ni sehemu ambayo ina hali ngumu sana kimazingira ukilinganisha na mabara mengine.

Aidha Dr. Kilahama alitumia fursa yake ya uwenyekiti kuwaomba na kuwakaribisha wajumbe wa mkutano wa 22 wa COFO kuiona Tanzania kama ni sehemu muhimu ya kutembelea kwa sababu kuna vivutio vingi ikiwemo mlima mrefu kuliko yote barani Afrika-Mlima Kilimanjaro (Come to Tanzania the land of Kilimanjaro). Wageni wengine walioweza kuongea wakati wa ufunguzi wakiongozwa na Dr. Kilahama ni pamoja na:
Mhe. Rosine Amane Baiwong Djibergui, Waziri wa Kilimo na Mazingira nchini Chado ambaye pia ni Rais wa COMIFAC;
Mhe. Shin Won-Sop, Waziri wa Misitu, Jamhuri ya Korea;
Mhe. Thomas Gass, Naibu Katibu Mkuu, Umoja wa Mataifa anayeshughulikia, Masuala ya Kiuchumi na Kijamii,
Mhe. Piet Vanthemsche, Rais wa AGRICORD, Ulaya na mwisho ni
Mhe. Jose Graziano da Silva, Mkurugenzi Mkuu FAO.


Baada ya wageni hao waalikwa kutoa hotuba zao Mwenyekiti Dr. Kilahamaalifunga shughuli za ufunguzi na hatimaye kuanzisha rasimi Mkutano wa 22 wa Kamati ya Misitu Duniani uliosadikiwa kuhudhuriwa na wajumbe Zaidi wa 600 kutoka nchi 120 na mashirika ya kimataifa 10.

Tanzania katika mkutano huo iliwakilishwa na wajumbe sita alioongozwa na Mhe. Balozi Msekela aliyefuatana na Afisa kutoka Ubalozini Bwana Ayoub. Kutoka Dar-Es-Salaam Wizara Ya Maliasili Na Utalii ni Bwana Zawadi Mbwambo aliyewakilisha Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Bwana Lyimo kutoka Wizarani. Pamoja na hao walihudhuria Prof. Yonica Ngaga, Mkuu wa Kitivo Cha Misitu na Uhifadhi Asilia na Dr. Laurence Mbwambo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI) yenye makao makuu katika Manispaa ya Morogoro.

Baada ya kufungua rasimi mkutano wa 22 wa COFO kwanza, Mwenyekiti aliwaomba wajumbe wapitishe rasimu ya Agenda za mkutano kitu ambacho walikifanya bila ya kusita. Pili, aliendesha Agenda iliyohusu uchaguzi kwa kuwathibisha Wenyeviti sita wa Makundi au mabara ili wawe Makamu wa Mwenyekiti wa COFO-22 ambayo kipindi chao cha uongozi kitaisha wakati wa mkutano kwa 23 wa COFO utakaofanyika 2016 mjini Roma.

Baada ya uthibitisho kufanyika ikawadia zamu ya kumchagua Mwenyekiti mpya ambapo wajumbe kwa pamoja Walimchagua aliyekuwa Rais wa Gayana, Amerika ya Kusini (kwa kipindi cha miaka 12 na aliwahi kuwaa waziri wa Fedha wa nchi hiyo kwa miaka sita) Mhe. Dr. Bharrat Jagdeo, kuwa Mwenyekiti wa COFO 22. Kwa tendo hilo hapo Mwenyekiti wa COFO 21 Dr. Felician Kilahama wa Tanzania alihitimisha uongozi wake katika chombo hicho muhimu cha kimataifa kwa niaba ya Bara la Afrika.
All the contents on this site are copyrighted ©.