2014-06-26 13:56:32

Siku ya kuombea Utakatifu wa Mapadre!


Wapendwa taifa la Mungu, Tumsifu Yesu Kristu. Leo Mama Kanisa anasherehekea sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. RealAudioMP3

Moyo uliochomwa mkuki pale msalabani. Kumbe Mama kanisa anasherehekea chemchemi ya neema za Mungu. Sherehe hii ni kati ya sherehe za Bwana kadiri ya mpango wa kilitrujia ambayo huja kila Ijumaa ya pili baada ya sherehe ya Pentekoste.

Mara moja tunaposikia neno Moyo Mtakatifu wa Yesu, tunapaswa kukumbuka maneno ya Mt Yohane, asemaye “tazama jinsi Mungu alivyoupenda ulimwengu”. Na hivi bila kubabaika tunatambua kuwa ni mapendo ya Mungu kwa wanadamu wote na kwa vizazi vyote. Kanisa likitafakari zawadi hiyo kubwa ya mapendo ya Mungu kwa wanadamu wote, haliachi kutumia zawadi hiyo kusogeza karibu neema za Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa mapadre wake, ndiyo kusema leo pia ni sikukuu ya kutakatifuzwa kwa mapadre.

Wapendwa taifa takatifu, tukiwa na nia njema tumfuase Bwana tukitafakari Neno lake ambalo Mama Kanisa ametuwekea leo hii ili kwalo tutambue mapendo ya Mungu yatokayo katika Moyo wake. Katika somo la kwanza Mungu anaongea na Waisraeli kwa njia ya Musa. Anawaambia jinsi alivyowapenda, akisema sikulazimishwa na awaye yote wala kitu chochote, wala wingi wenu, wala uzuri wenu katika kuwapenda ninyi, bali uthabiti wa moyo wangu na makusudio makamilifu yaliyo katika moyo wangu tangu milele.

Baada ya tangazo la mapendo ya Mungu kwa Waisraeli Musa anawaalika wapokee mwaliko huo mtakatifu kwa kuishika sheria ya Mungu na hukumu zake. Wote twajua kuwa "sheria ya Mwenyezi Mungu ni kamilifu, humpa mtu uhai mpya…" Zab. 19:7 Huo ndio mwitiko wa mkristo na awaye yote katika kupokea mapendo yatokayo katika Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Mwinjili Matayo anakazia mwaliko huo kwa kuonesha matokeo ya mapendo ya Mungu kwetu. Akisema njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha" Mt 11:28. Kumbe wale wote watakao itika mwaliko huu watapumzik katika Moyo wa mapendo kwa kuondolewa mizigo yote yenye kuleta udhaifu wa roho na mwili. Pamoja na hilo Mwinjili anakazia pia jambo la unyenyekevu na upole wa moyo na anatualika kutambua kuwa mahali pekee pa kujifunza ni katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambaye amefunua pendo la Mungu.

Mwinjili Yohane katika kutangaza upendo wa Mungu anafundisha akisema ili mmoja aweze kupokea mwaliko wa mapendo, yampasa kusadiki kabisa katika Mwana wa Mungu aliye ndani ya Baba, na kwa namna hiyo Mungu atakuja ndani yake. Anaweka wazi fumbo la umwilisho wa Mwana wa Mungu, upendo halisi yaani Mungu anapomtoa Mwanae wa pekee kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Kwa umwilisho, Mungu anaitazama dunia katika mtazamo chanya, na anaingia katika historia ya maisha ya watu aliowapenda milele.

Mtaguso mkuu wa Pili wa vatican katika ile Hati ya kichungaji juu ya Kanisa katika ulimwengu "Gaudium et Spes" unawaalika waamini kuitazama dunia katika mtazamo chanya na kuweka chachu ya Injili kama Kristu alivyoweka chachu ya mapendo kwa njia ya umwilisho wake. Kwa sababu hiyo, leo Kanisa linasali kwa kuuelekea Moyo Mtakatifu wa Yesu ili mapendo ya moyo huo yakae ndani ya ulimwengu na ulimwengu huu uwe ni mahali pema pa kuishi.

Baada ya tafakari toka Neno la Mungu naomba tuchukue maneno machache katika lugha yetu ya kila siku yatusaidie katika kutambua mwelekeo wa mwanadamu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Daima Nasikia watu wakisema "Jamaa yule ana moyo" na labda nawe umesikia! Unalo swali juu ya hili? Mimi nina swali “ mbona watu wote wana mioyo?

Kwa vyovyote vile hapa kuna jambo la ziada ambalo haligusiki, natumai si moyo wa nyama bali moyo wa mahusiano mema na watu wengine na hivi moyo wa mapendo ya kimungu. Katika kuendelea kufuatilia nimesikia pia watu wakisema "jamaa yule ana moyo mkuu" ndiyo kusema anao moyo wa kustahimili, kutafakari na kuvumilia mateso yampatayo katika maisha yake. Si hayo tu bali nimesikia "jamaa yule ana moyo mpole" kwa jinsi hiyo jamaa huyu anao moyo wa mapendo yatokayo katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, maana Bwana mwenyewe amesema "mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo”

Mpendwa msikilizaji, tokana na tafakari hii, kama mmoja atakuuliza nini maana ya Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, mara moja sema sikukuu ya Mapendo ya Mungu kwa Wanadamu wote, Sikukuu ya kuwatakatifuza mapadre. Ni sikukuu ya upendo upeo utokao kwa Mwenyezi Mungu.

Mama Kanisa amechagua sikukuu hii iwe ni kwa ajili ya kuwatakatifuza mapadre ili wajazwe neema na baraka tele kwa ajili ya kazi yao ya kichungaji inayodai mapendo ya kimungu. Kwa neema na baraka hizi taifa lote la Mungu litatakatifuzwe. Kumbe ni sikukuu ya kutakatifuzwa pia kwa waamini wote, maana mapadre si kwa ajili yao wenyewe bali kwa ajili ya uchungaji uliojazwa nguvu ya Kimungu.

Wanatakatifuzwa ili waweze kukaa katika kifua cha Bwana na wavumilie utume wao mpaka wanapofikisha taifa la Mungu katika Yerusalem mpya. Wanatakatifuzwa ili maisha yao yawe ni chachu kwa maisha ya watu, yawe ni ekaristia mkate umegwao katika jumuiya kama asemavyo Mtakatifu Ursula.

Tunaalikwa basi leo kuwaombea mapadre wote na Wanaushirika wa Moyo Mtakatifu wa Yesu ulimwenguni kote, ili maisha yao yawe changamoto kwa taifa zima la Mungu. Tunawatakieni heri na baraka tele zitokazo katika Moyo Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.