2014-06-26 12:01:58

Kuporomoka kwa thamani ya Kwacha Zambia ni janga kwa wananchi!


Askofu mkuu Telesphore Mpundu wa Jimbo kuu la Lusaka, Zambia anasema Kanisa litaendelea kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa linapenda kuona kwamba, wananchi wote wa Zambia wanahudumiwa barabara kadiri ya Katiba, sheria na kanuni za nchi bila upendeleo.

Ni dhamana ya watunga sera na wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanachukua hatua madhubuti katika kupanga na kutekeleza sera ambazo zitawasaidia wananchi wa Zambia kuwa na nguvu ya kiuchumi, kuliko ilivyo sasa kiasi kwamba, wananchi wengi wanaendelea kukata tamaa kutokana na mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma baada ya thamani ya fedha ya Zambia kuendelea kuporomoka katika soko la fedha.

Askofu mkuu Mpundu anasema, ikiwa kama maskini wanaendelea kutumbukia katika umaskini, hapa kuna walakini katika utawala, kwani sera na mikakati ya kiuchumi haina budi kuhakikisha kwamba, inawasaidia watu kujikwamua kiuchumi, pale lengo hili linaposhindwa kufikiwa, Serikali haina budi kuketi na kuangalia upya mikakati na sera zake za kiuchumi.

Askofu mkuu Mpundu ameyasema haya hivi karibuni wakati wa mahojiano na gazeti moja nchini Zambia kuhusu hali ya umaskini wa wananchi wa Zambia. Kanisa katika utume wake wa kinabii, linapenda kuishauri Serikali ya Zambia kuangalia sera na mikakati yake ya kiuchumi ili iweze kusaidia kuchangia mchakato wa maboresho ya wananchi wa Zambia. Imeandikwa kwamba, “mtawatambua kwa matunda yao”.

Serikali ya Zambia haina budi kubuni mikakati ya kuimarisha fedha yake, vinginevyo watu wataendelea kuteseka kutokana na kushuka kwa thamani ya Kwacha ya Zambia. Kanisa litaendelea kutekeleza utume wake wa kinabii kwa kuishauri Serikali pale inapoona inafaa, ili kukuza na kudumisha misingi ya utawala bora kwani hapa Kanisa na Serikali linawahudumia Wazambia: kiroho na kimwili, kumbe kuna haja ya kushauriana, kusikikizana na kujadiliana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Zambia katika ujumla wao!.








All the contents on this site are copyrighted ©.