Taka za plastiki zinazoishia baharini zinasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira
kiasi hata cha kuhatarisha maisha ya viumbe hai baharini, utalii pamoja na sekta ya
uvuvi. Haya yamebainishwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia mazingira
uliofunguliwa rasmi tarehe 23 Juni na unatazamiwa kuhitimishwa hapo tarehe 27 Juni
2014.
Bidhaa ya plastiki zina nafasi ya pekee sana katika maendeleo ya mwanadamu,
lakini pia zinachangia kwa kiasi kikubwa uharibu wa mazingira, jambo ambalo haliwezi
kamwe kufumbiwa macho! Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP linasema kuna
haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta mbinu mkakati utakaodhibiti uchafuzi wa mazingira
unaosababishwa na taka za plastiki.
Umoja wa Mataifa unasema, kuna haja ya
kupunguza matumizi yake, kuzitumia au kuzigeuza na kuwa bidhaa nyingine. Lengo ni
kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaofanywa na taka za plastiki, jambo linaloweza kuwa
ni mzigo mkubwa katika ukuaji wa uchumi. Mkutano huu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira
unahudhuriwa na wajumbe kutoka katika nchi 160 wanachama wa UNEP, kwenye Makao makuu
ya UNEP, Nairobi, Kenya.