Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii,
anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali
kwa ajili ya kuziombea Jumuiya za Kikristo huko Mashariki ya kati zinazokabiliwa na
hali ngumu ya maisha, ili ziweze kuendelea kuishi mahali ambapo Ukristo umepata mizizi
na chimbuko lake!
Taarifa zinaonesha kwamba, akaunti ya Baba Mtakatifu Francisko
kwenye mtandao wa kijamii ujulikanao kama twitter imefikia wafuasi zaidi ya millioni
kumi na nne, wanaojipambanua kwa matumizi ya lugha tisa za kimataifa. Itakumbukwa
kwamba, akaunti hii kwa mara ya kwanza ilifunguliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
XVI kunako tarehe 3 Desemba 2012.