Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete Jumatatu, Juni 23,
2014 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China
Mheshimiwa Li Yuanchao ambaye yuko katika ziara rasmi ya siku sita katika Tanzania.
Mheshimiwa Yuanchao aliwasili nchini Jumamosi, Juni 21, 2014.
Mheshimiwa Yuanchao
ambaye amefuatana na mawaziri wanne amekutana na Rais Kikwete, Ikulu, Dar Es salaam,
baada ya kuwa amekutana na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Makamu wa Rais,
Mohammed Gharib Bilal ambayo pia yamefanyika Ikulu.
Katika mazungumzo kati
ya Rais Kikwete na Mheshimiwa Yuanchap, viongozi hao wawili wamejadili hali ya uhusiano
wa kihistoria kati ya nchi hizi mbili na Rais Kikwete ameishukuru China akisema kuwa
bado Tanzania inatarajia kupata wawekezaji kutoka China, kupata masoko ya Tanzania
kuuza bidhaa zake katika China na kuendelea kupata misaada na mikopo ya maendeleo
kutoka nchi hiyo. Rais Kikwete pia ametumia muda kuweza kuishukuru China kwa ushirikiano
wake katika kuchangia maendeleo ya Tanzania ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya TAZARA
iliyokamilika mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Rais Kikwete pia ametaja miradi mikubwa
mingine ambayo imeungwa mkono na China ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bomba ya gesi
kutoka Mtwara hadi Dar es salaam, mradi mpya wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na miundombinu
yake, ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa ambao unaendelea na maendeleo ya miradi
ya chuma na makaa ya chuma ya Liganga na Mchuchuma.
Rais Kikwete pia ameishukuru
China na taasisi zake kwa kufikiria kugharimia miradi mingine kama vile ujenzi wa
chuo kikuu cha kilimo kitakachoitwa Julius Nyerere Agricultural University kilichopangwa
kujengwa Butiama na ujenzi wa maghala makubwa ya kuhifadhi nafaka kufuatia kuongezeka
kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini.
Mwezi uliopita wakati akihudhuria
Mkutano wa Taasisi ya Uchumi Duniani (WEF) Kanda ya Afrika mjini Abuja, Nigeria, Rais
Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa China.