Kanisa linafundisha kwamba, kazi inayo nafasi kubwa katika mchakato wa maboresho ya
maisha ya mwanadamu kiroho na kimwili. Watu wanapaswa kuheshimu na kuithamini kazi
halali inayowapatia riziki yao ya kila siku. Kazi inajumuisha na kukamilisha hali
ya mwanadamu japokuwa kazi sio lengo peke yake katika maisha.
Kwa njia ya
kazi mwanadamu anaufanya ulimwengu kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kusimamia
mafao ya wengi. Mababa wa Kanisa wanasema, utu wa mwanadamu ndicho kipimo cha heshima
ya kazi.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao
ya kijamii anasema kwamba, anatamani kuwaona watu wengi zaidi wakiwa wanafanya kazi
inayoheshimu na kuzingatia utu wa mwanadamu.