Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linasema kwamba, linaunga mkono jitihada za kidiplomasia
katika kutafuta muafaka na hatimaye, amani ya kudunu nchini Iraq ambayo kwa sasa inakabiliwa
na machafuko makubwa ya kisiasa, kiasi cha kusababisha maafa kwa watu wasiokuwa na
hatia.
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linasema, haliungi mkono kamwe
vita huko Iraq kwani historia inaonesha kwamba, hakuna suluhu ambayo imepatikana kwa
njia ya mtutu wa bunduki matokeo yake ni kwamba, watu wanaendelea kupoteza maisha
siku hadi siku. Serikali ya Marekani inawajibika mbele ya wananchi wa Iraq, ili kusaidia
kujenga serikali ya umoja wa kitaifa, ili wananchi wa kawaida waweze kujisikia kuwa
ni sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu. Ili kufikia lengo hili, wananchi wote
wa Iraq hawana budi kushirikishwa kikamilifu.
Uvamizi na vita iliyoendeshwa
nchini Iraq kwa kusaidiana na Jeshi la Marekani limepelekea wananchi kugawanyika katika
misingi ya kidini, hali ambayo imechangia kuibuka kwa watu wenye misimamo mikali ya
kiimani. Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani inasema kwamba,
ingependa kuona suluhu ya amani inapatika Nchini Syria, vita ambayo inaonekana kusahauliwa
na Jumuiya ya Kimataifa. Majadiliano ya upatanisho wa kitaifa na misaada ya kibinadamu
ni mambo msingi yanayoweza kuchangiwa na Marekani katika medani za kimataifa!