2014-06-24 09:37:20

Adhimisheni Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa Ibada, uchaji na nidhamu!


Askofu mstaafu Mathias Josefu Isuja wa Jimbo Katoliki Dodoma, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu Dekania ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jumapili tarehe 22 Juni 2014 amewataka waamini kuhakikisha kwamba, wanajiandaa kikamilifu ili waweze kushiriki katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Waamini wajenge utamaduni wa kuchunguza dhamiri na kuungama dhambi zao ili kujipatanisha na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani kabla ya kushiriki Mwili na Damu Azizi ya Kristo, chakula cha kiroho, mkate wa uzima wa milele ulioshuka kutoka mbinguni. Kwa mtu anayeshiriki Sakramenti ya Ekaristi Takatifu bila ya kufanya maandalizi ya kina anakula hukumu yake mwenyewe!

Siku kuu ya Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, mafumbo yanayoendelezwa na Mama Kanisa, kila wakati waamini wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kumbe, hili ni Fumbo la Imani, ambalo waamini wanaalikwa kuliadhimisha kwa Ibada, Uchaji na Nidhamu. Ekaristi Takatifu ni kiini na chemchemi ya imani, changamoto kwa waamini kutokubali kuyumbishwa hata kidogo. Waamini wawe tayari kumpokea Yesu wa Ekaristi na tayari waoneshe ujasiri wa kumpeleka kwa wengine, wao wenyewe wakijitahidi kuwa kweli ni Ekaristi kwa jirani zao.

Imeandaliwa na
Rodrick Minja,
Dodoma.







All the contents on this site are copyrighted ©.