2014-06-23 09:39:08

Watu millioni mbili wanakabiliwa na baa la njaa Mali


Watoto zaidi ya laki tano wenye umri chini ya miaka mitano nchini Mali wanakabiliwa na tatizo kubwa la utapiamlo na kwamba, watu zaidi ya millioni moja na nusu wako hatarini kukumbwa na baa la njaa nchini humo, ikiwa kama hatua za dharura hazitaweza kuchukuliwa mapema na Jumuiya ya Kimataifa. Tahadhari hii imetolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kibinadamu na kwamba, kwa sasa hali ni mbaya sana!

Asilimia 85% ya watoto wanaokabiliwa na lishe duni nchini Mali ni wale wanaotoka maeneo ya Mali Kati na Kusini, sehemu ambazo shughuli za uzalishaji katika sekta ya kilimo bado hazijaweza kukidhi mahitaji ya lishe bora kwa wananchi walio wengi. Uzalishaji wa mazao ya nafaka umepungua kwa kiasi kikubwa, wakati huo huo bei ya mazao ya chakula imeongezeka maradufu kutokana na kinzani na machafuko ya kijamii yaliyojitokeza nchini humo kuanzia mwaka 2012 na mwaka 2013.

Wakimbizi na wahamiaji walioanza kurejea tena kwenye makazi yao baada ya hali ya kisiasa kutulia wamejikuta wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Hali hii imechangia ongezeko kubwa la kiwango cha utapiamlo kadiri ya taarifa zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani, WHO, hivi karibuni.







All the contents on this site are copyrighted ©.