Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo.
Kisha kuadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu, ambamo tulimtukuza na kumshangilia Mungu
katika Utatu, sasa tumeadhimisha sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo, tunamshangilia
Kristo aliye kifungo cha Upendo na Ishara ya Umoja.
Kristo Yesu
amependa kukaa kwetu katika Sakramenti Takatifu sana ya EKaristi. Neno linasema “nao
walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake,
akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu. Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa,
akisema, Kunyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo
kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi” Mt. 26:26-28.
Na pengine amesema
“ Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba
yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.
Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili
nilipo mimi, nanyi mwepo” Yoh. 14:1-3.
Kristo Yesu alipokuwa akiwaaga wanafunzi
wake kabla ya kupaa kwake, aliahidi kurudi ili awakaribishe kwake. Kristo Yesu ametimiza
neno hilo kwa uwepo wake katika Neno na Sakramenti. Kristo yupo nasi katika Neno lake,
yupo nasi katika Sakramenti zake. Zaidi sana, yupo nasi katika Sakramenti ya Ekaristi
Takatifu. Mafundisho ya imani yetu yanasema hivi: katika Sakramenti nyinginezo zote,
tunapokea neema za Kristo ili zitusaidie kupata wokovu. Tunapokea nguvu ya Kristo.
Lakini katika Sakramenti Takatifu sana ya Ekaristi, tunampokea Kristo Yesu mwenyewe
katika mwili wake na damu yake, katika Umungu wake na Ubinadamu wake.
Kuanzia
nyakati za Kanisa la mwanzo kabisa, kumekuwa na maadhimisho ya Karamu hii kuu, kwa
ukumbusho wa Bwana kama alivyoagiza mwenyewe. Kadiri nyakati zilivyokwenda na uelewa
wa mafumbo ya Kristo ulivyokuwa, Ibada rasmi zilianza kuwekwa, ikiwa ni pamoja na
maandamano, ili kuweza kushuhudia hadharani Imani yetu kwa Yesu wa Ekaristi, huku
tukikiri kuwa yeye ndiye mfalme wa maisha yetu, ni mwalimu wetu na kiongozi wetu,
yupo kati yetu akituongoza kwenda kwa Baba.
Mashangilio ya sherehe hii, tulipaswa
kuyafanya siku ya Alhamisi kuu. Lakini kwa sababu za kichungaji, kwamba hatuwezi kufanya
mashangilio mazito kipindi kile cha Kwaresma, ili kutuacha tutafakari kwa kina zaidi
fumbo la mateso ya Kristo, Mama Kanisa ametuwekea siku maalumu baada ya Sherehe ya
Utatu Mtakatifu, tuweze kusherehekea hadharani na kukiri imani yetu kwa Yesu wa Ekaristi
waziwazi.
Kwa nini tunaandamana na Kristo Yesu wa Ekaristi kwa mashangilio
makubwa hivi? Maana yake ni hii: Sisi hapa duniani ni Kanisa linalosafiri, Kanisa
linalohiji. Na katika safari yetu hii, kuna mawimbi na mitikisiko mbalimbali ambayo
huweza kukwamisha kabisa safari yetu ya kwenda kwa Baba. Tunaandamana tukiwa na Yesu
wa Ekaristi tukiwa tunaungama kwamba, safari yetu hii ya kwenda kwa Baba, itakuwa
salama endapo tu, tutakuwa tayari kuwa na Yesu, kuwa tayari kuongozwa na Neno lake,
kuwa tayari kurutubishwa na Sakramenti zake.
Hivyo, yale maandamano ya Sherehe
ya Mwili na Damu ya Kristo, ndiyo muhutasari wa maisha binafsi mwamini. Swali ambatanishi
hapa ni hili: katika safari ya maisha yako unaongozwa na nini? Nani anayaongoza maisha
yako? Dira yako haswa ni nni? Na lengo la safari yako ni nini? Hapo tunaalikwa kutafakari
kwa uzito zaidi juu ya uwepo wa Kristo Yesu katika maisha yetu ya kila siku.
Tukiligeukia
Kanisa la nyumbani, yaani familia tutashududia kwamba, familia zetu kama Kanisa dogo
la nyumbani linapata mitikisiko mibaya mno, inayowapelekea wanafamilia kukata tamaa
ya kendelea kusafiri pamoja kuelekea ukamilifu. Na hakuna anayefurahia mitikisiko
hiyo. Dawa ni nini? Ni Yesu wa Ekaristi, tumpokee katika Neno lake, neno lake lituongoze,
tumpokee katika Sakramenti zake, akae katika mioyo yetu, akae katika familia zetu,
awe nasi maishani mwetu mwote.
Katika famili zetu, tusipokuwa tayari kumwinua
Yesu na kuongozwa naye katika upendo wake, katika unyenyekevu wake, katika huruma
yake, katika msamaha wake, katika uvumilivu wake, katika haki yake na katika imani
yake, hapo hatuwezi kuwa salama. Wengi wetu badala ya kumwinua Yesu na kuambatana
naye, tunaambatana na tamaa za mali na mafanikio, tunaambatana na mioyo inayotamani
vita, tunainua juu tabia zetu mbaya, tunainua ngumi na kelele za matusi badala ya
kumwinua Yesu, na hapo ndipo unapozuka moto wa fujo ndani ya familia, hadi kupelekea
safari ya pamoja kuvunjika.
Sherehe hii na mashangilio yake vinatukumbusha
sote tuwe watu wa Kiekaristi. Familia zetu ziwe za Kiekaristi, parokia zetu ziwe za
Kiekaristi, Majimbo yetu yawe ya Kiekaristi. Tukubali sote kuongozwa na Yesu wa Ekaristi,
Mungu wa upendo na Mfalme wa amani anayetuongoza katika safari yetu hii ya kumwendea
Mungu.
Mwisho tutoe rai ya kichungaji kwetu sote tunaoliungama jina la Kristo
Yesu ndani ya Kanisa Takatifu. Kila mmoja afanye jitihada kubwa ya akili, mwili na
roho ili kulinda imani na heshima kuu kwa Sakramenti takatifu sana ya Ekaristi. Nguzo
mbili muhimu sana kwa imani yetu ni NENO la MUNGU na Sakramenti Takatifu sana ya Ekaristi.
Tukijiruhusu kuchezacheza na Neno la Mungu, au kuchezacheza na Ekaristi Takatifu,
hapo tunacheza na misingi, hatutabaki salama. Tuungane pamoja na makuhani wetu, kudhibiti
kabisa hila zote na kufuru zinazotendwa dhidi ya Sakramenti Takatifu sana.
Nasi
sote, tupende kumpokea Kristo Yesu katika Sakramenti ya Mwili na damu yake, katika
hali njema ili tupate uzima tulioahidiwa. Lakini pia tukwepe kabisa tabia ya kumpokea
pasipo kustahili: mwenyewe alisema, tukifanya hivyo, tunakula hukumu. Hatupati amani,
faraja na kitulizo rohoni, wala uzima endapo tunampokea katika hali ya kufuru.
Pamoja
na hayo, tunaalika na kuhimiza sana, tupende kuiabudu Sakramenti ya Ekaristi takatifu.
Tuketi miguuni pake, tumwage mioyo yetu mbele yake, tumpatie furaha zetu na uchungu
wetu, tumpe mipango ya maisha yetu aibariki, tumpe pia mapungufu na kushindwa kwetu
ili atuinue, tumpe marafiki zetu na wapendwa wetu awabariki, tumpe pia maadui zetu
na watesi wetu awaguse kwa neema zake, tumtegee sikio la moyo, tulisikie neno lake
katika ukimya mtakatifu, naye yupo tayari anatungoja, atusikilize. Yesu ni rafiki
wa pekee asiyechoka kutusikiliza.
Ibada kwa Ekaristi Takatifu ni kiini cha
Ibada zote katika Kanisa. Ibada nyingine zote zinatuelekeza kwa Yesu. Ibada kwa Yesu
wa Ekatisti inatupatia muungano kamili naye mwenyewe aliye njia, ukweli na uzima.
Tenga walao nusu saa tu katika wiki, ukamwabudu Yesu wa Ekaristi, ukishazoea utaweza
kufanya zaidi, na utaonja heri ya kuwa karibu na Yesu, na usikose kuwaalika wengine
kwenda kwa Yesu.
Kutoka studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin
Mkorwe, OSB.