2014-06-23 08:17:13

Amani ya kweli inakumbatia hakijamii!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani, ILO hivi karibuni, limejadili kuhusu ajira safi miongoni mwa vijana wa Misri, tukio ambalo liliwajumuisha vijana kutoka dini ya Kiislam na Kikristo. RealAudioMP3

Tukio hili lilipembua kwa kina na mapana kuhusu athari za ukosefu wa fursa za ajira nchini Misri na mikakati inayoweza kutumika katika mchakato wa kutengeneza fursa za ajira zinazozingatia ubora wa kazi kati ya vijana wa Misri, ili kutekeleza haki ya kufanya kazi, kuendeleza ulinzi wa kijamii pamoja na kukuza majadiliano ya kijamii.

Takwimu zinaonesha kwamba, vijana wanaunda asilimia 70% ya idadi ya watu ambao hawana ajira nchini Misri, kati yao ni wale waliohitimu shule za sekondari, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu. Tukio hili liliongozwa na viongozi wa kidini kutoka Kanisa la Kikoptik na Kiislam kwa kuwashirikisha wadau wengine wa maendeleo ya vijana nchini Misri.

Shirika la Kazi Duniani, ILO linaunga mkono juhudi za Jumuiya za Kidini katika kuhimiza tunu msingi za maisha ya kijamii, maadili na utu wema. Kwa kushugulikia fursa za ajira, ILO inapania pia kuchochea amani kwani Shirika hili lina amini kwamba, hakuna amani pasi na haki jamii.

Kwa upande wao, viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wanabainisha kwamba, majadiliano ya kijamii yanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji, tija na maendeleo katika nyanja mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Kongamano hili ni sehemu ya hija iliyoamriwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika mkutano wake mkuu wa kumi, uliofanyika mwishoni mwa Mwaka 2013.

Viongozi wa Kanisa la Kikoptik wanasema kwamba, majadiliano ya kidini na kiekumene ni muhimu sana katika ujenzi wa tunu msingi za maisha ya kijamii, kwa kukazia umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, kwa kutambua kwamba, licha ya tofauti zao za kiimani, lakini wote ni ndugu wamoja wanaounda taifa la Misri.

Maendeleo ya kweli yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili ni muhimu sana hata kwa waamini wa dini ya Kiislam, wanapotekeleza mapenzi ya Mungu. Viongozi wa kidini wamekubaliana kimsingi kwamba, wataendeleza juhudi hizi hata kwa siku za usoni kwa ajili ya maendeleo ya vijana wa Misri.








All the contents on this site are copyrighted ©.