Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa anakusudia kurejea darasani kushika tena
chaki kwa kuwa mhadhiri kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi National Defence College
(NDC) cha Dar Es Salaam. Rais Kikwete amelieleza hilo Ijumaa, Juni 20, 2014, wakati
alipotoa Mhadhara (Lecture) kuhusu Usalama wa Taifa (The Security of the Nation) mbele
ya wanafunzi wa Chuo hicho kilichoko Kunduchi, Dar Es Salaam.
Rais Kikwete
amewaambia wanafunzi wa kozi ya pili ya Chuo hicho kutoka nchini na nchi za jirani
za Uganda, Kenya na Rwanda: “Najisikia mwenye raha sana kuweza kurudi darasani kutoa
mhadhara huu. Tukio hili linanikumbusha enzi zangu katika Chuo cha Kijeshi cha Monduli
(TMA). Ni matarajio yangu pia kuwa nitaweza kurudi kuwa mhadhiri katika Chuo hiki
baada ya kukamilisha kazi yangu ya sasa.” Rais Kikwete ambaye alizungumza kwa kiasi
cha saa mbili, alianza mhadhara wake baada ya kupata maelezo kuhusu maendeleo ya Chuo
hicho na baadaye akajibu maswali ya wanafunzi ambao walimwuuliza kuhusu mambo mbali
mbali yanayohusiana na usalama wa nchi.
NDC kilianzishwa rasmi Septemba 2,
mwaka 2012 na Chuo hicho kilizinduliwa na Rais Kikwete Septemba 10, mwaka 2012 wakati
alipotembelea Chuo hicho kwa mara ya kwanza kufuatia juhudi kubwa za uongozi wake
kuhakikisha kuwa chuo cha namna hiyo na cha aina yake kinaanzishwa nchini. Rais pia
alifungua kozi ya kwanza ya Chuo hicho.
Kundi la wanafunzi wa kwanza kwenye
Chuo hicho lilimaliza mafunzo yake Julai 23, mwaka 2013 na sasa chuo hicho kinaendesha
kozi ya pili yenye wanafunzi 30. Chuo hicho tayari kimepata usajili kamili wa NECTA
ambako kina uwezo wa kutoa shahada ya uzamili katika masomo ya Strategic Studies.